Dkt. Mwanjelwa baada ya kuteuliwa wizara ya Utawala Bora, aomba jambo hili kwa watumishi



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) ameahidi kushirikiana na watumishi wa ofisi yake kupanga mikakati endelevu itakayowezesha kutoa huduma bora kwa umma na kuhakikisha ofisi hiyo inakuwa na mtazamo chanya katika kuwahudumia wananchi.

Dkt. Mwanjelwa ametoa ahadi hiyo leo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bo ra mara baada ya kuripoti ofisini kwake jijini Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Dkt. Mwanjelwa ameomba ushirikiano wa dhati kutoka kwa watumishi wa ofisi yake kwani kila mtumishi ana mchango na umuhimu wake katika kuboresha utuoaji wa huduma kwa umma.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Naibu Waziri mwenye dhamana ya utumishi na utawala bora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alimteua Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tarehe 10 Novemba, 2018 na kumuapisha tarehe 12 Novemba, 2018.