Jeshi la Polisi laua tena watuhumiwa ujambazi


JESHI la Polisi Wilayani Muheza Mkoa wa Tanga limeua watuhumiwa watatu wa ujambazi wakiwa na bunduki aina ya gobore, wakijaribu kuvamia nyumba ya mfanyabiashara.

Tukio hilo ni la pili kwa mwezi huu polisi kuua watuhumiwa wa ujambazi. Novemba 15 majira ya usiku polisi mkoani Mwanza waliwaua watuhumiwa sita wa ujambazi kwa kuwapiga risasi katika mapambano.

Jeshi la Polisi limesema watu hao waliuawa wakati wa majibizano ya risasi na askari.

Imeelezwa kuwa watu hao walivamia nyumba ya mfanyabiashara huyo, Jackson Mhufu, kwa lengo la kupora fedha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Ngwaru Kanisani Kijiji cha Ngwaru Kata ya Masuguru wakati watu hao walijiandaa kupora nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Bukombe, watuhumiwa hao walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wakitumia gari ndogo nyeusi aina ya Nissan, huku wakiwa na bunduki aina ya gobore pamoja na vifaa vya kuvunja mirango vilivyokuwa katika mabegi.

Bukombe alisema watu hao waliingia Muheza wakitokea mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kufanya uhalifu.

Bukombe alisema kuwa majambazi hao walipofika nyumbani kwa Mhufu, wananchi waliwatilia shaka ndio wakatoa taarifa
kwa Jeshi la Polisi ndipo wakajipanga kukabiliana na majambazi nao kisha kuwaua wakati wa kukabiliana nao. Lilikuwa ni tukio la pili la uvamizi nyumbani kwa mfanyabiashara huyo.

Baadhi ya mashuhuda ambao walikuwa katika eneo hilo wakiwa kwenye ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushirika wa Ngwaru, walisema kuwa walisikia milio ya risasi mfululizo ndipo walishtuka na kutoka nje ya kanisa kushuhudia kuna tukio gani.

Walisema walishuhudia majambazi hao wakiwa wameuawa na askari polisi.

Mashuhuda hao ambao walikuwa wamefurika katika eneo la tukio, huku watuhumiwa hao wa ujambazi wakiwa wamekufa baada ya kupigwa risasi na polisi, walisema ni mara yao ya pili kufanya jaribio la kupora katika nyumba ya mfanyabiashara huyo.

Rajabu Juma, mkazi wa Majengo aliwapongeza askari na maofisa wa polisi wilaya ya Muheza kwa kufanya kazi nzuri ya kupambana na uhalifu.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items