KUFUTIA vifo vya wasichana wawili vilivyotokea katika kata ya matundasi wilayani Chunya, mkoani Mbeya ambao walitumbukia na kufia katika moja ya mashimo yaliyoachwa wazi na wachimbaji, Mkuu wa wilaya ya Chunya, MaryPrisca Mahundi, amebuni mpango mkakati wa kuhakikisha mazingira ya uchimbaji katika wilaya yake yanalindwa na kuhifadhiwa ili kuepusha madhara kwa wananchi na mifugo.
Akizungumza baada ya kutembelea moja ya mashimo yaliyosababisha mauti kwa wasichana hao, Mahundi alisema kuna kila
sababu ya kuwabana wachimbaji kufanya kazi zao kwa kuzingitia weledi ili kuepusha athari zitakanazo na shughuli za uchimbaji.
Alisema serikali ya wilaya imejipanga kuhakikisha mazingira yanatunzwa, kulindwa na yanaboreshwa ili kupunguza na ikibidi kutokomeza kabisa athari hasi zitokanazo na uchimbaji wa madini.
“Wachimbaji lazima wachimbe kulingana na taratibu na sheria zilizopo na pia wahakikishe wanafukia mashimo hayo wamalizapo shughuli za uchimbaji kwa kuwa mashimo hayo yanapoachwa wazi husababisha vifo vya mara kwa mara vya watu na mifugo,” alisema.
Aliwaagiza wataalamu wa mazingira kutembelea na kuchukua hatua kali za kisheria kwenye maeneo yote ya uchimbaji na kuhakikisha kuwa sheria na taratibu za kimazingira zinafuatwa ili kulinda maisha ya watu na mifugo.
Jamillah Ramadhani Chaka, mwanajiolojia katika ofisi ya Madini Wilayani Chunya, alisema kumekuwa na ukiukwaji wa sheria kwa baadhi ya wachimbaji, hivyo kufanya toauti na vibali vyao walivyopewa na Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
“Sheria zinasema mtu yeyote anayetaka kuchimba lazima awasilishe muhtasari wake kutoka NEMC ambao unaweka wazi kwamba mwekezaji atachimba kulingana na sheria ya mazingira na baada ya kuchimba atarudisha mazingira kama yalivyokuwa mwanzoni ili kulinda mazingira na vyanzo vya maji,” alisema Jamillah.
Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali inayotetea uhifadhi wa mazingira wilayani Chunya, Lucas Malangalila, alisema kuna madhara makubwa yanayosababishwa na wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakichimba hata katika maeneo ya vyanzo vya maji.
“Athari ni kubwa hususani kwa uchimbaji unaofanyika katika vyanzo vya maji na tumejipanga kufanyia kazi changamoto katika maeneo yote ya vyanzo vya maji ambapo wachimbaji wameacha mashimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya mji wa Makongarasi, tutafukia mashimo na kupanda miti.”
