Klabu 5 zenye ukuta mgumu zaidi duniani

SAFU imara ya watu wanne nyuma ndio ambayo kila timu inaihitaji kuweza kumaliza matatizo ya ulinzi. Timu kama Atletico Madrid na Bayern Munich zimejihakikishia kuwa na uhakika wa kuizuia safu yoyote ya ushambuliajia ya timu pinzani.

Hakika, safu ya ulinzi ndio sehemu inayoanzia na unapomalizikia mpira kwa timu yoyote ya mpira wa miguu. Safu nzuri ya ulinzi ndio yenye uwezo wa kuanzisha au kuvunja kikosi cha kwanza cha wachezaji 11.

Klabu za mpira wa miguu hivi karibuni zimevunja rekodi nyingi, kuanzia kwenye dirisha la usajili na dimbani. Uwezo wa kuzuia mashambulizi ya timu pinzani ndilo jukumu muhimu zaidi kwa watu wanne wa nyuma wanaotakiwa kulifanya, na timu hizi tano zimeweza kuwa na safu imara zaidi za ulinzi hadi sasa msimu huu.

Kwa sasa, timu hizi zimeweza kuruhusu mabao kwenye ligi zao, lakini ndizo zilizoonesha kuwa na safu ngumu zaidi ya ulinzi duniani kwa sasa.

5. Liverpool

Tangu kuwasili kwa Mholanzi Virgil Van Dijk msimu uliopita, Liverpool imekuwa na nguvu kubwa na kiwango kisichoshuka katika safu ya ulinzi duniani. Ikiwa imefungwa mabao manne tu hadi sasa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, wekundu hao wameonyesha kuwa hakuna safu ya ushambuliaji inayoweza kuwapita kiurahisi.

Kwa uwapo wa Joe Gomez na Dejan Lovren, safu ya ulinzi ya Liverpool imeonyesha mfano jinsi gani mabeki wanavyotakiwa kupangwa.

Huku Van Dijk akiwa kiongozi wa ulinzi, Gini Wijnaldum mara kwa mara ameonekana akicheza vizuri nyuma kwa ushirikiano na Lovren au Gomez, wakitengeneza safu imara ya wachezaji watatu, na kuwaruhusu mabeki wa kushoto, Trent Alexander-Arnold na Andy Robertson kupanda na kwenda kusaidia mashambulizi. Kwa safu hii ya ulinzi waliyonayo Liverpool kwa mara nyingine tena wana nafasi kubwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England, EPL.

4. Manchester City

Manchester City inajulikana kwa nguvu yake kwenye ulinzi, huku kwenye benchi wakiwa na wachezaji wengine imara zaidi. Kwa kumuongeza Aymeric Laporte hivi karibuni, safu ya ulinzi ya City ndiyo inayoonekana kukamilika zaidi. Wakongwe Nicolas Otamendi na Vincent Kompany wanacheza mara kwa mara na wamekuwa mabeki muhimu mno kwa historia ya klabu hiyo.

Huku John Stones na Laporte wakiwa chaguo la kwanza la Guardiola msimu huu, wamekuwa na uwezo wa kuzuia mashambulizi ya timu yoyote wanayocheza nayo.

Fernandinho anaongeza ulinzi kwenye safu ya kiungo, na amekuwa akizuia mipira yote ya eneo la kiungo huku kuna wakati akisukumiza mashambulizi mbele. Mabeki wa pembeni Mendy na Walker nao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya City.

3. Barcelona

Wamekuwa hawana kiwango kizuri zaidi kwenye safu ya ulinzi duniani, lakini Barcelona ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga wakiwa wameruhusu kufungwa mabao 12. Ukweli ni kwamba uwezo wa mabeki wa kati ndiyo umeifanya safu yao ya ulinzi kuimarika, huku La Blaugrana hao wakiwa na safu imara zaidi ya ushambuliaji na kuwa na mafanikio ya kuzuia mashambulizi langoni mwao.

Gerard Pique wakati akiwa kiongozi wa mabeki wa nne wa nyuma, Sergio Busquets mara kwa mara amekuwa akitengeneza mfumo mzuri kwa kucheza vizuri zaidi na Umtiti au Clement Lenglet.

Jordi Alba akiwa anacheza zaidi beki ya kushoto, huku Sergi Roberto, ambaye anacheza kiungo ya katikati, safu ya ulinzi ya Barcelona imekuwa na ukuta imara dhidi ya timu pinzani. Mechi yao ya hivi karibuni ya El Clasico dhidi ya Real Madrid ilithibitisha kwamba, msimu huu wanaweza kufanya kweli kwenye kuwania taji la Ligi ya mabingwa Ulaya na wanaweza kutwaa mataji matatu.

2. Chelsea

Baada ya kuwasili kwa Maurizio Sarri mfumo wa ‘kupaki basi’ umefufuka hapo kwenye dimba la Stamford Bridge. Wote David Luiz na Antonio Rudiger wamekuwa na ushirikiano mzuri zaidi kwenye safu ya ulinzi na kuwafanya mashabiki wa Chelsea kuwa na furaha kila wanapowaona. Ili kuifanya safu yao ya ulinzi kuwa ngumu zaidi, viungo wa kati, N'golo Kante na Jorginho wamekuwa kiungo muhimu zaidi kwa kuzuia mashabulizi na kupeleka mashambulizi kwa washambuliaji.

Kikosi hicho msimu huu hadi sasa kimeruhusu kufungwa mabao saba kwenye Ligi Kuu kabla ya mechi ya jana na kuwa na mwanzo bora zaidi wa msimu tangu ule wa 2016/17 wa Ligi Kuu England. Kitu cha muhimu zaidi msimu huu ni kwamba pia wapo kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Europa.

1. Atletico Madrid

Safu ya ulinzi isiyovunjika, ndio wanavyoitwa, wakati Atletico Madrid ikiwa imeimarisha zaidi ulinzi tangu kutua kwa kocha, Diego Simeone. Huku wakiwa na mabeki wao imara zaidi, Jose Gimenez na Diego Godin, wamethibitisha kwamba ni mabeki wawili bora zaidi duniani. Ingawa wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, wameruhusu kufungwa mabao matano tu kwenye ligi msimu huu.

Mabeki wa pembeni nao wametoa mchango muhimu zaidi katika kuiimarisha safu yao ya ulinzi. Lucas Hernandez na Santiago Arias wameonyesha kuwa imara na kufanya safu hiyo ya nyuma ya wachezaji wanne kuwa ngumu mno kwa timu pinzani kuipita au kutengeneza mashambulizi kirahisi.

Wameonyesha kuwa wana uwezo mzuri zaidi wa kulilinda lango lao kutoka kwa timu pinzani kwenye Ligi Kuu ya La Liga.