Picha ya mtandao
Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila, ameagiza madereva hao kukamatwa na Jeshi la Polisi kisha kupelekwa katika Gereza la Kilimo la Songwe, kwenda kufanya kazi ya kulima katika mashamba hayo kwa muda usiopungua miezi sita ili wajifunze kufuata sheria.
Alitoa agizo hilo wakati wa mikutano yake ya kusikiliza kero za wananchi katika kata mbalimbali za Jiji la Mbeya, alidai kuwa madereva hao wakiacha bila kuchukuliwa hatua hizo wataendelea kusababisha ajali na kulisababishia taifa hasara.
Chalamila alisema ajali za bodaboda zimekuwa zikisababisha vifo kwa madereva hao, abiria wao pamoja watumiaji wengine wa barabara hali ambayo husababisha kupungua kwa nguvu kazi ya taifa huku wengine wanaopata madhara hayo wakiwa hawana hatia.
Alisema ikiwa wataachwa taifa litaendelea kupoteza nguvu kazi kwa kuwa vijana wengi wanapoteza maisha na wengine wanabaki na ulemavu wa kudumu kutokana na ajali za bodaboda.
Alisema mbali na vifo hivyo, watu wanaachwa na ulemavu wa kudumu na hivyo kuongezeka kwa kundi la wategemezi ambao hawawezi tena kuzalisha mali kama ilivyokuwa awali.
Alisema serikali haitawavumilia madereva hao, huku akilitaka Jeshi la Polisi kusimamia sheria za usalama barabarani na kuhakikisha kuwa zinafuatwa na kila mtumiaji wa barabara.
"Ninakerwa sana na hawa vijana wa bodaboda, wanaendesha pikipiki utadhani kesho hawafiki, wanahatarisha maisha yao pamoja na watumiaji wengine wa barabara hivyo sisi kama serikali hatuwezi kuona vijana wetu wanaendelea kufa," alisema Chalamila na kuongeza.
"Hawa mkiwakamata inabidi tuwapeleke darasani kidogo ili wakajifunze kule hata kwa muda wa miezi sita na darasa lao litakuwa ni Gereza la Kilimo la Songwe, wakimaliza tunawauliza kama wamejifunza wakikiri tunawaachia ikiwa bado tunawaongezea," aliongeza.
Aidha, Chalamila alisema kazi ya kuendesha bodaboda ni kazi kama ilivyo kazi zingine hivyo aliwataka waiheshimu kwa kuwa inawaingizia kipato kwa ajili ya mahitaji ya kila siku.
Alisema bodaboda ni sekta ambayo imetoa ajira kwa vijana wengi, lakini imekuwa ni janga, kwa kuwa vijana wengi wamepoteza maisha na wengine wamebaki na ulemavu kutokana na ajali ambazo zinasababishwa na uzembe.
Hata hivyo, alisema hataki kusikia tena ajali za bodaboda ambazo zinasababishwa na mwendo kasi na kuwasihi madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
