Makala: AY na Victoria Kimani kuendeleza ushikaji wao

Muimbaji kutokea nchini Kenya, Victoria Kimani kwa sasa yupo Tanzania kwa ajili ya kufanya media tour. Hii ni baada ya kuachia ngoma yake mpya unayokwenda kwa jina la Highest Calibre.

Hata hivyo imebaika kuwa kuna kolabo kati ya AY na Victoria Kimani ingawa bado haijajulikana ni lini itaoka. Aliyedokeza hilo ni meneja wa AY, Sallam SK.

AY amekuwa akifanya kolabo na wasanii wengi wa Kenya, mara ya mwisho AY kushirikiana na msanii wa nchini humo ni pale alipotoa wimbo uitwao More & More akiwa na Nyashinski.

Wasanii wengine wa Kenya ni kama Amani ambaye walitoa nyimbo kama Usiwe Mbali na King na Queen, Avril kwenye wimbo No Stress. Msanii mwingine ni Jaguar ambaye alimshirikisha AY kwenye wimbo unaokwenda kwa jina la Nimetoka mbali, wimbo huo ndio ulimtangaza Jaguar kimuziki zaidi.

Pia alitoa wimbo uitwao Asante akiwa na Dela ambao ulifanya vizuri kwa kiasi kikubwa kwa upande wa Afrika ya Mashariki.

Kama ulikuwa hujui Dela ndiye yule muimbaji aliyefanya cover ya wimbo Hellow wa Adele kutoka nchini Uingereza kwa lugha ya kiswahili, wimbo wake (cover) ulifanya vizuri sana kwenye baadhi ya vituo vya radio nchini Marekani.

Kabla ya Sasa

victoria Kimani ameshafanya kazi na wasanii kadhaa wa Tanzania kama Diamond Platnumz na Ommy Dimpoz walipotoa wimbo uitwao Prokoto uliotoka miaka minne iliyopita, ni kipindi ambacho Victoria alikuwa akifanya muziki wake chini ya lebo ya Chocolate City.

Utakumbuka kuna wakati AY alikuwa akiwasimamia wasanii kupitia Menejimenti yake ya Unit Entertainment ambapo aliwasaini wasanii kama Stereo na Ommy Dimpoz.

Stereo akiwa chini ya Unit Entertainment aliweza kumshikisha Victoria Kimani kwenye wimbo wake uitwao Wako (Never Let You Down) uliotoka mwaka 2014. Hivyo kolabo ya AY na Victoria Kimani inakuja kuendeleza ule urafiki wao wa kikazi uliyokuwepo toka hapo awali.