Makamu wa Rais azindua Jeshi USU la wanyamapori na Misitu leo


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa wadau wote wa uhifadhi hususani jeshi letu USU kuhakikisha kuwa wanatekeza kwa azma moja nia njema ya Serikali ya kuhakikisha usalama wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na misitu.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo leo wakati wa sherehe za uzinduzi wa Jeshi Usu la Wanyamapori na Misitu iliyofanyika katika eneo la Fort Ikoma Serengeti mkoani Mara.

“Vilevile, nitoe rai kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uhifadhi kuheshimu sheria za nchi, kutoa ushirikiano kwa jeshi usu na kuwa raia wema kwa kujiepusha na kuacha mara moja kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya uhifadhi ikiwemo kuingiza mifugo, kuanzisha kilimo, makazi na ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na matumizi mengineyo,” alisema Makamu wa Rais.

Utalii umekuwa moja ya vyanzo vikubwa vya kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwa asilimia 25% na pato la Taifa kwa asilimia 17% pamoja na kutoa  ajira rasmi na zisizo rasmi.

Mfumo huu mpya wa kusimamia maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na misitu utasaidia kumaliza ujangili kabisa.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye amesema wanatambua ukubwa wa tendo hili la uanzishwaji wa jeshi la Usu kwa faida ya nchi, kwa faida ya kizazi hiki na kizazi kijacho.

“Tunaamini kwamba pamoja na ujasiri na uzalendo lakini operesheni za jeshi hili zitafanyika kuzingatia ubinadamu ili tuwafanye wananchi waone umuhimu wa rasilimali hizi ushirikiano wao katika kuzilinda na kuzitunza ni muhimu” alisema Mwenyekiti huyo.