Jumatatu hii,ilikuwa ni siku ya maswali na majibu bungeni mjini Dodoma ambapo wabunge mbalimbali wameuliza maswali na kujibiwa na serikali. :Tazama mambo muhimu kwa ufupi yaliyotolewa na serikali.
1. Utaratibu wa watu wanaosafiri katika vyombo vya usafiri majini kuwa na vitambulisho wakati wa kukata tiketi na wakati wa kupanda chomboni ni utaratibu muhimu ambao unapaswa kuendelea kwa sababu unalinda usalama wa abiria, mali, meli na uchafuzi wa mazingira- Naibu Waziri Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa
2. Serikali kupitia TANROADS inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpanda-Ugalla- Kaliua- Ulyankulu- Kashishi- Ushetu- Kahama yenye urefu wa km 428 ikihusisha na usanifu wa daraja la Ugalla ambapo kiasi cha shilingi milioni 912.979 kimetengwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 kwa ajili ya kazi hiyo-Naibu Waziri Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa
3. Vigezo vinavyotakiwa kuajiri vijana katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kwa mujibu wa Kanuni ya 5.01 ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Juzuu ya Kwanza ( Utawala) Kifungu cha (1) kinachoeleza sifa za kuandikishwa ikiwemo awe raia wa Tanzania, Asiwe mwanachama wa chama chochote cha siasa, awe na tabia nzuri, awe na umri usiopungua miaka 18 na kutimiza masharti mengine yote ambayo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi anaweza kuyatoa- Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa- Dkt. Hussein Mwinyi
4. Malengo ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa malighafi zinazopatikana kila mkoa zinaongezwa thamani kabla ya kuuzwa yakiwemo mazao ya Kilimo, hivyo Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imekuwa ikihamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa Viwanda katika maeneo ambayo malighafi za kutosha zinapatikana Mhe. Anthony Mavunde.
5. Serikali kupitia Kituo cha uwekezaji (TIC) inaendelea kuhamasisha waagizaji wa mafuta ya kula wakiwemo East Coast Oils& Fats, Mkoani Edible Oil& Detergents Ltd, Murzah Wilmar E.A Industries na BIDCO kuanzisha viwanda vya kusindika mafuta kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini- Mhe. Anthony Mavunde
6. Serikali imeondoa kodi na tozo mbalimbali katika mazao ya kilimo likiwemo zao la alizeti pamoja na kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa mafuta ghafi na asilimia 35 kwa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje ya nchi ili kuhamasiha uwekezaji katika sekta hii- Mhe. Anthony Mavunde
7. Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu( REA III) mzunguko wa kwanza katika maeneo mbalimbali nchini- Naibu Waziri, Mhe. Subira Mgalu
8.Serikali imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali na kukusanya taarifa za kiutawala ili kupata takwimu na sababu zinazochangia ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto nchini- Waziri Ummy Mwalimu.
9. Kwa sasa Serikali inashughulikia uboreshaji wa viwanja vingi nchini ili vifike kiwango cha Uwanja wa Nyamagana, naishauri Halmashauri ya Jiji la Mwanza itumie njia zingine kama vile kuwahamasisha wadau wa michezo na kushirikiana nao kufanikisha lengo la kujenga majukwaa ya Uwanja huo bila kuisubiri Serikali- Naibu Waziri, Mhe. Juliana Shonza
10. Hali ya Viwanja vingi vya michezo nchini ni mbaya hivyo nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote washirikiane na Halmashauri zetu, Vyama vya michezo na wadau mbalimbali wa michezo kuchangia katika kuboresha miundombinu ya michezo nchini na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya michezo- Naibu Waziri, Mhe. Juliana Shonza.
