Mamlaka za maji zatakiwa kuimarisha huduma



Naibu Waziri wa  Maji, Jumaa Aweso amezitaka Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha kuwa zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma ya majisafi na salama katika maeneo yote.

Akizungumza wakati akifunga Kikao kazi cha siku mbili kwa watendaji wakuu wa Mamlaka za Maji na wahandisi amesema kuwa  wanalo jukumu kubwa la kutekeleza majukumu yote kwa weledi na kuimarisha huduma za maji kwa wananchi.

“Kwa yoyote atakayejaribu kuturudisha nyuma katika kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hatutaweza kumvumilia kwa namna yoyote zaidi yakumuweka pembeni," Alisisitiza Aweso.

Akifafanua Aweso amesema kuwa watendaji hao wanatakiwa kuhakikisha kuwa sekta  ya maji inachochea maendeleo na ustawi wa wananchi.

Pia alizitaka Mamlaka za maji kutangaza miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuonesha juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa sekta ya maji ina mchango mkubwa katika kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda inayosisitizwa na Serikali  ya Awamu ya Tano.