https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mbaroni kwa tuhuma za ubakaji mtoto wa miaka 6 | Muungwana BLOG

Mbaroni kwa tuhuma za ubakaji mtoto wa miaka 6


Jeshi la Polisi mkoani Kagera, linamshikilia Nelson Petro (18), kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alisema tukio hilo lilitokea kijiji na kata ya Maruku katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na polisi walipata taarifa juzi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

"Taarifa iliripotiwa hapa kituoni, mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alifika na kueleza kwamba Novemba 5, mwaka huu saa nne usiku akiwa nyumbani kwake, aligundua tatizo hilo wakati akimwogesha," alisema.

Alisema mtoto huyo alipiga kelele kuwa anaumia sehemu za siri na mama yake alipomhoji alimweleza kuwa aliingiliwa katika sehemu zake za siri na kijana huyo, ndipo akaamua kutoa taarifa.

Alisema kuwa mtoto huyo alipelekwa hospitali kwa ajili ya vipimo na uchunguzi zaidi na baada ya taarifa ya madaktari ilithibitishwa kuwa mtoto huyo ameingiliwa katika sehemu zake za siri.

Kamanda huyo aliwataka wazazi kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuwaepusha kukumbwa na madhara kama hayo, huku akiitaka jamii pia kuachana na fikra potofu zinazosababisha kufanya uhalifu huo.

"Jambo hili pamoja na kuwa la kisheria haliruhusiwi, bado sio jema na halifai kijamii na kiimani, maana wananchi wana dini zao ambazo zinapinga masuala kama hayo," alisema.

Kamanda huyo alisema kuwa majibu ya madaktari ndiyo yatatoa mwanga wa hatua gani zifuate.