https://monetag.com/?ref_id=TTIb Wafugaji na Wakulima wapewa wiki tatu kumaliza mgogoro | Muungwana BLOG

Wafugaji na Wakulima wapewa wiki tatu kumaliza mgogoro


MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Maryprisca Mahundi, amewapa wiki tatu wafugaji wa kijiji cha Igundu katika kata ya Sangambi wilayani humo kuhamisha mifugo yao kuipeleka katika kijiji cha Paris ambacho kimetengwa kwa ajili ya wafugaji.

Alitoa agizo hilo juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo ambapo alisema lengo la kuondoa mifugo hiyo ni kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja kuokoa chanzo cha maji ambacho wakazi wa eneo hilo wanakitegemea.

Alimwagiza Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Joseph Nangale, kusimamia na kuhakikisha mifugo hiyo inahamishwa huku akimtaka kutumia nguvu iliyotumika kuwazuia wakulima kufanya shughuli zao karibu na chanzo cha maji.

Mahundi alisema amechoshwa na migogoro ya wakulima na wafugaji katika kijji hicho cha Igundu na kwamba agizo lake hilo ni la mwisho na kwamba atakaporudi tena kwenye kijiji hicho na kukuta inaendelea hakutakuwa na majadiliano tena na kwamba wasije wakamlaumu.

“Mkae chini mjadiliane na mkubaliane idadi ya mifugo ambayo kila mfugaji wa kijiji hiki atatakiwa kubaki nayo hapa, nimewapa siku 10 viongozi wenu waniletee taarifa ya majidiliano hayo, lakini nimewashauri kila mfugaji abaki na mifugo 10,” alisema Mahundi.

Alisema idadi hiyo aliyopendekeza kila mfugaji abaki nayo kijijini hapo ni rahisi kuimudu ili isiingie kwenye mazao ya wakulima na kwamba itasaidia kumaliza migogoro.

Mahundi alisema baadhi ya wafugaji wamekuwa na tabia ya kuingia kwenye vijiji wakiwa na idadi ndogo ya mifugo kisha baada ya muda wanaenda kuchukua mingine walikotokea ama kuinunua kwenye magulio na kuijaza kuipeleka kwenye vijiji hivyo hali inayosababisha ongezeko kubwa la mifugo kwenye maeneo husika.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Nangale alikiri kijiji hicho kuwa na idadi kubwa ya mifugo kuliko uwezo wa eneo la kijiji hicho hali ambayo inasababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.

Alisema migogoro hiyo ilikuwa inaibuka baada ya mifugo kuwashinda wafugaji na kuingia kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na hivyo kuwafanya wakulima waanze kutaka kulipiza kisasi.

Aliahidi kushirikiana na halmashauri nzima ya kijiji hicho katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya la kuondoa mifugo na kwamba watayashirikisha makundi yote ili kufikia mwafaka ambao hautaleta shida.

“Kijiji cha Paris kina eneo kubwa kwa ajili ya mifugo na ni eneo rafiki kwa sababu hakuna mwingiliano na shughuli zingine za kibinadamu, tulikitenga maalumu kwa ajili ya wafugaji,” alisema Nangale.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya aliwatahadharisha viongozi wa vijiji wanaopokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili waingize mifugo kwenye vijiji vyao kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria endapo watabainika.

Alisema baadhi ya wafugaji wamekuwa na tabia ya kuuza mifugo yao na kuwahonga viongozi wa vijiji na kwamba hata ikiibuka kesi kati ya wakulima na wafugaji, wafugaji wamekuwa wakiwahonga viongozi ili washinde kesi hizo.