Nyati wafa maji katika jaribio la kumkimbia Simba

Mamia ya nyati wamekufa maji katika mto wa mpakani kati ya Botswana na Namibia.

Uchunguzi wa awali unaashiria kuwa wanyama hao walikuwa wakifukuzwa na simba wakakimbilia mtoni.

Mmiliki wa hoteli karibu na mto huo ameiambia BBC kuwa nyati hao walikwama kwasababu kingo za mto zilikuwa juu sana hali iliyowafanya wanyama hao kukanyagana hadi kufa.

Mamlaka nchini Botswana inakadiria kuwa karibu nyati 400 walikufa katika kisa hicho.

Watu wanaoishi karibu na mto huo walijipatia kitowea cha nyama nyama na kujipelekea nyumba .

Simone Micheletti, ambaye ni mmiliki hoteli moja upande wa mpaka wa Namibia, anasema idadi ya wanyama hao ilikuwa kubwa kupita kiasi.

Bwana Micheletti ameiambia BBC kuwa simba walisikika wakinguruma sana usiku wa Jumanne.

''Niliposhuka mtoni asubuhu ya Jumatano niliona mamia ya nyati wakiwa wamekufa.

Ameongeza kuwa usiku wa Jumanne ulikuwa na mawingu ya mvua ambayo huenda ilikinga mwangaza wa mwezi ambao hutumiwa sana na wanyama nyakati za usiku.

Wizara ya mazingira ya Botswana imetoa taarifa kuelezea kuwa hiki si kisa cha kwanza cha wanyama kufa maji katika mto Chobe.

Lakini bwana Micheletti amesema idadi kubwa kama hiyo ya wanya kufa maji haijawahi kushuhudiwa.