Singida United yatarajia kujiimarisha kwa mkopo


LICHA ya kupitia wakati mgumu kwa sasa, uongozi wa klabu ya Singida United umepanga kukiimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji wengine kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Novemba 15, mwaka huu, lakini ikilenga zaidi wachezaji wa mkopo.

Singida inapitia wakati mgumu wa kiuchumi uliosababisha kukimbiwa na baadhi ya wachezaji wake akiwamo golikipa Manyika Peter aliyetimkia Kenya.

Mbali na Manyika, Singida United pia wamekimbiwa na mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu, Dany Lyanga na kiungo Mudathir Yahaya waliojiunga na Azam FC.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa klabu hiyo, Festo Sanga, alisema wanajiandaa kufanya usajili, lakini watawachukua wachezji kwa mkopo ili kukiimarisha kikosi chao.

Alisema wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya klabu kuwachukua baadhi ya nyota wake ambao wanapanga kuwaacha kwenye dirisha hilo dogo la usajili.

“Tunataka kukiimarisha kikosi chetu, tutasajili wachezaji si chini ya wawili kwa ajili kuongeza nguvu…, ni kweli tumepitia kipindi kigumu kiuchumi, lakini tunapambana kuhakikisha timu inafanya vizuri,” alisema Sanga.

Mkurugenzi huyo alisema watachukua baadhi ya wachezaji kutoka kwa mabingwa wa soka nchini, Simba.

Kikosi hicho cha Singida kinashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya  kujikusanyia pointi 18 kufuatia kucheza michezo 14 mpaka sasa.

Mpya zaidi Nzee zaidi