Watu 12 wameuawa katika mauaji California

Takriban watu 12 wameuawa akiwemo afisa wa polisi katika kilabu moja ya burudani kwa jina Thousand Oaks, California.

Takriban watu 200 waliripotiwa kuwa ndani ya kilabu ya Borderline and Grill wakati wa shambulio hilo.

Maafisa wanasema mshukiwa huyo alipatikana amefariki ndani ya eneo hilo la burudani na bado hawajamtambua. Hawajui lengo lake la kutekeleza kisa hicho.

Sherehe ya muziki wa aina ya country music miongoni mwa wanafunzi ilikuwa ikiendelea wakati mshukiwa huyo ambaye alikuwa amevalia nguo nyeusi, alipoingia katika baa hiyo na kuanza kufyatua risasi.

Ripoti zinasema kuwa huenda mshukiwa huyo alitumia maguruneti ya moshi na bunduki inayojulikana kwa jina handgun kulingana na walioshuhudia.

Mtu mmoja aliyekuwa amejeruhiwa aliambia runinga ya KTLA: Tulilala chini tulisikia watu wakipiga kelele. rafiki yangu ndio DJ hivyobasi alisitisha muziki tulisikia kelele nyingi.

Shahidi mwengine , Teylor Whittler, alisema: "Nilikuwa katika sakafu ya kucheza densi na nikasikia milio ya risasi , hivyobasi niliangalia nyuma na mara nikasikia kila mtu akisema laleni chini.

"Tulibabaika , kila mtu alisimama , niligongwa na kuanguka, niliwachwa katika sakafu hadi mtu mmoja alipokuja na kunivuta akinitoa nje.

Watu wengine walitoroka baa hiyo kwa kutumia viti ili kuvunja madirisha huku wengine wakijificha ndani ya vyoo.

Mkuu wa kikosi cha polisi wa mji wa Ventura Geoff alielezea kisa hicho ndani ya baa hiyo kuwa cha 'kutisha' na kusema kuwa kulikuwa na ''damu kila mahali''.

Anasema kuwa waokoaji waliwasili katija eneo hilo la mkasa dakika tatu baada ya wito wa dharura kutoka eneo hilo kutolewa.

Sharifu wa Ventura sajenti Ron Helus , ambaye alifariki baadaye akiwa hospitalini, alijaribu kuingia katika eneo hilo pamoja na afisa aliyekuwa akipiga doria katika barabara kuu.

Afisa huyo mwenye mtoto mmoja alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi na alitarajiwa kustaafu mwaka ujao.

''Alifariki kama shujaa. Aliingia kuokoa maisha ya watu wengine'', alisema Sharifu huyo.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa walipata bunduki ndani ya baa hiyo na kumpata mshukiwa akiwa amefariki. wanaamini huenda alijiuwa lakini bado hawajathibitisha.

Bado haijulikani waathiriwa wengine 11 ndani ya baa hiyo, lakini sherehe hiyo ya muziki wa country ni maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu.