Watumishi TRC mbaroni kwa tuhuma za magendo

WATU wanne ambao ni watumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kusafirisha zaidi ya mbao 1,000 kinyume cha utaratibu.

Watu hao hawakuwa na nyaraka zozote za usafirishaji wa mzigo huo.

Mbao hizo zilikamatwa jana majira ya saa 11 asabuhi zikitokea Tabora kwenda Mwanza, zikiwa kwenye mabehewa mawili ya treni ya mizigo, huku juu yake zikiwa zimefunikwa magodoro kwa lengo la kuficha maliasili hizo za serikali.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule, alisema baada ya kupewa taarifa na wasamaria wema juu ya usafirishaji huo wa mbao kinyemela, waliweka ulinzi mkali na hatimaye kuzikamata zikiwa kwenye treni hiyo ya mizigo.

"Jeshi la Polisi tunawashikilia watumishi wanne wa TRC kwa kusafirisha mbao kinyume cha utaratibu, bila kuwa na nyaraka zozote na vitu vingine zikiwamo pikipiki na asali zikiwa zimefunikwa na magodoro juu kwa ajili ya kuzificha," alisema Haule.

"Upelelezi ukikamilika watu hawa watapelekwa mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria na sasa hivi majina yao hatuwezi kuyataja kwanza kwa sababu za kiuchunguzi kwa sababu huu ni mtandao mkubwa," alisema.

Naye Mshauri wa Maliasili na Mazingira mkoani Shinyanga, Billie Edmott, alisema baada ya serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma wa Misitu Tanzania (TFS) kuimarisha ulinzi barabarani, hatimaye wafanyabiashara wamebuni mbinu mpya.

Alisema baadhi ya mbao zilizokamatwa ni zile ambazo serikali imeshakataza miti yake kukatwa ukiwamo mninga na mkurungu na kubainisha kuwa kwa mujibu wa sheria, mbao hizo watazitaifisha na kuwa mali ya serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alitoa wito kwa watumishi wa serikali kuachana na vitendo vya kuhujumu uchumi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items