Dkt. Shein afanya mazungumzo mazito na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini


Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za Jamhuri ya Korea za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Sog Geum-yong, ambaye amefika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alimueleza Balozi Sog kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea ambao umeweza kusaidia kuimarika kwa sekta za maendeleo ikiwemo sekta hiyo ya kilimo ambapo tayari imejiandaa vizuri  kwa kuweka mazingira mazuri ya mradi huo kwa kuyatayarisha mashamba yapatayo 60.

Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua za Jamhuri ya Korea kusaini mradi wa miundombinu ya kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji hivi leo ni uthibitisho wa wazi kuwa nchi hiyo imeamua kwa makusudi kushirikiania na Zanzibar kivitendo.

Alieleza kuwa tokea nchi hiyo ianze ushirikiano na ushusiano wa kidiplomasia kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar mnamo miaka ya tisini, imeweza kutoa ushirikiano wake mkubwa kwa Zanzibar  kwa kuweza kusaidia miradi kadhaa ikiwemo kilimo, elimu, uvuvi na mengineyo ambayo imeweza kuimarisha sekta za maendeleo nchini.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Korea imeweza kusaidia katika ujenzi wa skuli ya kisasa ya Sekondari ya Kwarara ambayo pia, ina studio ya matangazo pamoja na vifaa mbali mbali vya habari kwa ajili ya mafunzo na kutoa elimu kwa wananchi.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa juhudi za Jamhuri ya Korea imeweza kusaidia kuanzishwa kwa kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki (marine hatchery), kaa na majongoo ya baharini huko Bait el Ras ikiwa ni jitihada za kuhakikisha sekta ya uvuvi, ufugaji, ajira kwa vijana sambamba na ukuaji wa uchumi vinaimarika  hapa Zanzibar.