Machinga wagomea agizo hili la RC


Wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la ‘Machinga’ ambao wamejenga vibanda vyao kuzunguka soko la kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya, wamezua vurugu wakigomea agizo la Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, linalowataka waondoe vibanda hivyo.

Wafanyabiashara hao wanatakiwa kubomoa vibanda vyao vya biashara na kuhamia katika eneo la Nanenane ambako wametengewa eneo la biashara na tayari zaidi ya vibanda 700 vimeshajengwa huko kwa ajili yao.

Mkuu wa Mkoa, Chalamila Jumamosi ya wiki iliyopita aliwaamuru wamachinga hao kuondoka katika eneo la Soko la Kimataifa la Mwanjelwa na kutoa muda kuwa hadi ifikapo Ijumaa ya wiki hii hatahitaji kuwaona tena katika eneo hilo.

Kufuatia agizo hilo, jana asubuhi Wamachinga hao walianza kufanya vurugu ikiwa ni pamoja na kufunga barabara ya Mfikemo kwa kuchoma mbao na mabanzi ambayo walikuwa wanayachukua kwenye vibanda walivyobomoa.

Katika vurugu hizo Wamachinga hao walisikika wakitoa maneno makali yakimkashfu Mkuu wa Mkoa kabla ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghafia (FFU) kuingilia kati na kuanza kuwatawanya, huku baadhi yao wakikamatwa.

Hata hivyo, wakati vurugu hizo zikifanyika, wafanyabiashara wenye maduka ndani ya soko walikuwa wameyafunga huku shughuli zote ndani ya soko hilo zikiwa zimesimama.

Baadhi ya wafanyabiashara hao, walidai kuwa eneo hilo la kuzunguka soko walipewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, ili wajenge vibanda kwa ajili ya kufanya biashara zao baada ya kuwaondoa katika hifadhi ya barabara, lakini sasa wanashangaa kuona ofisi hiyo hiyo tena inawataka waondoke.

“Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wetu kabla ya Chalamila ndiye aliyetuweka hapa, sasa tunashindwa kuelewa kwa nini tuondoke, sisi hatutaki kuondoka, kwanza sisi huyu mkuu wa mkoa hatumtaki,” alisema mmoja wa vijana waliokuwa wanafanya fujo.

Mwenyekiti wa Wamachinga hao, Jerry Mwatebela, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha wenzake kufanya vurugu bila kumshirikisha wakati tayari suala hilo wanalishughulikia kama viongozi.

“Natambua kuwa tumeamuriwa na Mkuu wa Mkoa tuondoke hapa, na sisi kama viongozi tunalishughulikia suala hili kwa njia za kistaarabu, kwa kuwa tumeshaandika barua kwenda Ofisi ya Rais ili waingilie kati, lakini wenzangu bila kunishirikisha nasikia wameanza kufanya vurugu, hili la vurugu limenisikitisha sana,” alisema Mwatebela.

Aliwataka wamachinga wenzake kuachana na vurugu hizo na badala yake watulie wakati wakisubiri majibu ya barua yao kutoka Ofisi ya Rais wakiamini kuwa huko watapata suluhisho la tatizo lao.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alisema kuwa kwa sasa hakuna vurugu katika eneo hilo isipokuwa ulinzi uliopo ni kwa ajili ya kusimamia ulinzi na usalama.

Alisema jeshi hilo litaendelea kutoa taarifa kadri hali itakavyokuwa inaendelea na kwamba wao wanachokifanya ni kusimamia utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa.