Machinjio yasiyokua na kiwango kufungwa Zanzibar

Na.Thabit Madai, Zanzibar.

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeahidi  kusimamia na kudhibiti ubora wa machinjio ya ng’ombe  ili kuhakikisha wananchi visiwani Zanzibar  wanapata chakula kilicho salama kwa afya zao.

Sambamba na hayo imesema na machanjio yatakayo bainika kuwa hayakukidhi viwango na ubora hatua kali za sheria zitachukuliwa ikiwemo kufungiwa kwa machinjio hayo ili kumlinda mlaji.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Khamis Ali Omar aliyasema hayo   baada ya ziara yake ya kutembelea  machinjio yaliyopo  Kinyasini,Donge-  Muwanda na Mahonda  katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kuangali mazingira na ubora wa machinjio hayo.

Alisema  juhudi za Serikali ya mapinduzi ya zanzibar kupitia Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) ni kuhakikisha wananchi wanapata chakula kilichoandaliwa katika ubora unaostahiki ambao utamlinda mtumiaji asipatwe na madhara. 

Alisema Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar walianzisha kanuni ya kuwataka wananchi wanaosafirisha nyama ya ngombe kwa ajili ya biashara kutumia gari maalum za kusafirisha kutoka machinjioni kwa lengo la kulinda usalama wa chakula hicho

Dkt. Khamis amezitaka taasisi zinazosimamia suala la uingizaji wa ngombe ikiwemo Idara ya Mifugo, na Kilimo Wakaguzi pamoja na vyombo vya ulinzi kuwa na mashirikiano ya pamoja ili kuhakikisha ngombe hawachinjwi katika mazingira hatarishi.

Diwani wa Wadi ya Mahonda Haji Fadhil Mkadam aliwaomba Wakala wa Chakula na Dawa kuwasaidia kumaliza ujenzi wa chinjio lao liweze kuanza kazi  ili kuepuka usumbufu na kuvunja sheria ya kuchinja ngombe katika sehemu zisizorasmi.

Wakala wa Chakula na dawa wanaendelea kulizuwiya Chinjio la Mahonda lisifanye kazi kutokana na kukosa mahitaji maalum yanayotakiwa kuwepo kabla ya kuanza kazi za kuchinja ng’ombe.

Mmiliki wa Chinjio la Kinyasini Abdalla Mohamed alisema  wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuhakikisha sehemu yake ya kazi iko katika mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli hizo.

Aliwashukuru wakaguzi wa chakula kufanya ziara za mara kwa mara kwa lengo la kuwapa maelekezo ya kuweka mazingira safi katika sehemu za machinjio.

 Awali Mkaguzi  wa Chakula Maulid Khamis Shaabani  wa chinjio la Kinyasini alisema wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kufuatilia usalama wa ng'ombe wanaofikishwa katika sehemu hiyo kwa ajili ya kuchinjwa na wakigundua kasoro wanazuia kazi isiendelee.