Makatibu wa siasa na Uenezi wametakiwa kuinadi ilani ya uchaguzi ya CCM 2015/2020



Na. Thabit Madai, Zanzibar.

MAKATIBU wa Siasa na Uenezi wa ngazi za Matawi na Wadi nchini wametakiwa kutangaza  Sera imara za Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayotekelezwa kwa ufanisi katika maeneo mbali mbali nchini ili jamii ijue kwa upana maendeleo yaliyofikiwa katika nyanja za kisiasa, kijamii na kichumi.

Rai hiyo ameitoa Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Mhe.Ali Suleiman Shihata leo wakati akifungua Mafunzo ya Siku moja ya kuwajengea Uwezo Makatibu wa Siasa na Uenezi wa Ngazi za Matawi na Wadi za CCM Wilaya ya Dimani Kichama yaliyofanyika Tawi la CCM Mwanakwerekwe Unguja.

Mwakilishi huyo aliwakumbusha Makatibu hao kwamba pamoja na majukumu mbali mbali waliyokuwanayo bado wana wajibu wa kutangaza na kueneza kwa kasi kubwa Sera za maendeleo zinazotekelezwa kwa vitendo katika maeneo yao  na Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.

Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya ustawi wa maendeleo na kijamii katika Sekta mbali mbali jambo linalotakiwa kufafanuliwa vizuri na Makatibu hao ili wananchi wapate kufahamu utekelezaji wa ahadi wa viongozi wao waliowapa ridhaa ya kuongoza nchi kupitia mfumo huru wa Kidemokrasia.

Katika maelezo yake Shihata aliwasisitiza Makatibu hao kuwa wabunifu na wenye kujituma katika kuibua masuala mbali mbali yatakayokijenga Chama Cha Mapinduzi Kisiasa na Kiitikadi, ili kiende sambamba na siasa za sasa zinazotatminiwa kwa maendeleo ya kiutekelezaji kuliko maneno mengi ya majukwaani.

“Nawapongeza Viongozi wa Chama wote walioshiriki katika kuandaa jambo kubwa kama hili la kuwapatia elimu na ujuzi Makatibu wetu, ambao baada ya Mafunzo haya watakuwa na uwezo mkubwa wa kuyatangaza mazuri yote yanayofanywa na Serikali na CCM sambamba na kufafanua Sera na kufanya Tafiti za maendeleo ya kisiasa katika ngazi zenu za kiutendaji.”, alisema Shihata.

Pamoja na hayo alitoa tahadhari kwa kuwataka Makatibu hao wasimamie utaratibu wa baadhi ya Watu wanaojitokeza wakitaka kupewa kadi za CCM bila kupitia mdarasa ya Itikadi wachunguzwe kama wana sifa ya kuwa makada wa kweli ama wana lengo la kupata kadi kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Aidha amewataka watendaji hao kuwa na msimamo imara usioyumba kwa kufanya kazi kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na wasifanye kazi kwa matakwa ya Watu binafsi, ambao wana nia ya kukwamisha mikakati ya maendeo ndani ya Taasisi hiyo na Serikali kwa ujumla.

Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Dimani Hassan Suleiman Jaku alisema Mafunzo hayo yanatokana na agizo la Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar ambayo baaba ya kuwapatia Mafunzo kama hayo Makatibu wa Siasa na Uenezi wa ngazi za Majimbo, Wilaya na Mikoa yote yaliyofanyika Juni 23, mwaka 2018, waliwaagiza Makatibu hao washuke ngazi za Matawi hadi Wadi kuwajengea uwezo Makatibu wa Siasa na Uenezi.

Alieleza kuwa Mafunzo hayo yatakuwa endelevu katika Wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha kazi za CCM zinafanywa kwa mujibu wa Taratibu za Kikatiba, Kanuni na Miongozo ya CCM, na zitekelezwe katika hali ya ufanisi wenye tija kwa wanachama wote.

Katika taarifa ya Mafunzo hayo ilieleza kuwa jumla ya Makatibu 47 wameshiriki katika mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wajiimarishe kiitikadi, kisiasa na kimkakati kwa lengo la kufanikisha kwa ufanisi mikakati mbali mbali ya Chama na Serikali zake.

Kupitia taarifa hiyo waliomba Watu wanaotaka kujiunga na CCM lazima wapatiwe mafunzo ya miezi katika Matawi yao na wasimamiwe na kufuatiliwa kwa karibu na wahusika.

Kwa upande wake Kada wa CCM Baraka Mohamed Shamte, Akitoa mada ya Kazi na wajibu wa Makatibu wa Siasa na Uenezi kwa Mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo jipya la mwaka 2017,amewataka viongozi hao kusoma na kuchambua kwa kina Katiba, Ilani na miongozo mbali mbali za Chama cha Mapinduzi ili wafanye kazi zao kwa kujiamini na kwa uhakika zaidi.

Alisema CCM itaendelea kuwa Taasisi bora ya kisiasa endapo viongozi na Watendaji wake watakuwa mstari wa mbele kufuata maadili na miiko ya uongozi kwa lengo la kujenga Chama bora chenye misingi imara ya kimaadili.

Akitoa mada ya Wajibu wa Viongozi na Watendaji wa CCM Kujiimarisha Kiitikadi na Kimkakati wa kuweza kujenga nguvu imara zaidi ya Mapambano ya ushindi , Kada wa CCM Mohamed Haji Hassan amesema kuwa kila mwachama wa CCM anatakiwa kuwa muadilifu anayeamini na kutetea misingi ya umoja, uzalendo na ukweli usiokuwa na shaka wakati wote.

Aliwambia Makatibu hao kuwa ushindi wa CCM utatokana na juhudi binafsi wa viongozi wanaofanya kazi za Chama kwa kufuata miongozo ya Kitaasisi inayobadilika kulingana na wakati kwa lengo la kusimamia mikakati ya maendeleo kwa kila vipindi tofauti vya uongozi.

Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ya Mfenesini Haji Abdallah Daima akitoa mada ya maandalizi ya mikutano ya hadhara pamoja na Itifaki na Ushiriki katika Mikutano, alisema Makatibu hao ni lazima wajue masuala ya itifaki na maandalizi ya mikutano na shughuli za Chama kwa lengo la kuepuka kasoro mbali mbali zinazoweza kuharibu shughuli za kisiasa.

Katika Mafunzo hayo zimetolewa Mada tano zikiwemo Kazi na wajibu wa Makatibu wa Siasa na Uenezi kwa Mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo jipya la mwaka 2017, ya Wajibu wa Viongozi na Watendaji wa CCM Kujiimarisha Kiitikadi na Kimkakati wa kuweza kujenga nguvu imara zaidi ya Mapambano ya ushindi , Maandalizi ya Vikao na uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu , maandalizi ya mikutano ya hadhara pamoja na Itifaki na Ushiriki katika Mikutano pamoja .