Mtanzania kusimamia fainali Wanawake leo

ALIYEWAHI KUWA MWENYEKITI WA CHAMA CHA SOKA CHA WANAWAKE TANZANIA, LINA KESSY

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Chama cha soka cha Wanawake Tanzania, Lina Kessy ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kusimamia mchezo wa Fainali ya Afrika kwa Wanawake.

Lina atakuwa Kamishna wa mchezo huo utakaochezwa leo kati ya timu ya taifa ya Nigeria dhidi ya Afrika Kusini.

Mchezo huo namba 16 utachezwa Accra Sports Stadium kuanzia majira ya saa 10:00 Alasiri.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), fainali hiyo itachezeshwa na mwamuzi kutoka Zambia, Glady Lengwe, atakayesaidiwa na Mwamuzi msaidizi namba moja kutoka Madagascar, Lidwine Rakotozafinoro pamoja na  mwamuzi msaidizi namba mbili kutoka Malawi, Bernadettar Kwimbira huku mwamuzi wa akiba akiwa Fatou Thioune.

Katika fainali hizo zinazomalizika leo, mwamuzi wa Tanzania, Jonesia Rukyaa alikuwa miongoni mwa waamuzi walioteuliwa kuchezesha fainali hizo ambapo alichezesha mchezo wa nusu fainali kati ya Afrika Kusini na Zambia.

TFF ilisema kuwakilishwa kwa Watanzania haokwenye fainali hizo ni ishara tosha kuwa waamuzi na viongozi wa soka wa Tanzania wana uwezo mkubwa wa kuchezesha na kusimamia mechi kubwa.