Serikali yatafuta wabangua Korosho



Serikali imeanza mchakato wa kupata wazabuni wa ndani na nje ya nchi wa kubangua korosho kwa lengo la kuharakisha uandaliwaji wake tayari kwa mauzo.

Akizungumza na waandishi wa habari  kwenye kikao kuhusiana na maonyesho ya siku nne ya bidhaa za viwanda vya ndani yanayoanza leo Sabasaba wilayani Temeke, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda alibainisha kuwa uhitaji wa ubanguaji wa korosho hizo ni mkubwa.

Kakunda amesema, kwa sasa viwanda vya hapa nchini vina uwezo wa kubangua tani 40,000 kwa siku huku uhitaji ukiwa ni mkubwa zaidi hasa kwa kipindi hiki ambacho serikali inanunua zao hilo.

Alisema, kutokana na hali hiyo serikali inaendelea kuimairisha viwanda vya ndani kwa kuvijengea uwezo wa kubangua kiasi kikubwa cha korosho na wakati huo huo ikiendelea kuwasaka wazabuni hao.

Katika kuhakikisha hatua ya serikali ya kununua korosho inawanufaisha wakulima, waziri huyo alibainisha kuwa zaidi ya walanguzi 20 wa korosho za wakulima wamefikishwa mahakamani.

Alisema, wakati Serikali ikinunua korosho kwa Sh 3,300 kwa kilogramu, kuna walanguzi wamenunua korosho kwa Sh 600 na wanazipeleka kuuza kwa Serikali Sh 3,300 na vyombo vya dola vinawakamata.

Alisema: Rais John Magufuli hakufanya kosa kununua korosho kwa shilingi 3,300 lengo lake ni mkulima anufaike, sasa hao wanaolangua kwa wakulima na kuja kuuza kwa bei ya juu lazima wakomeshwe.

Alitoa mwito kwa walanguzi waliolangua korosho za wakulima kuwarejeshea korosho zao pamoja na fedha ili wakulima hao wakaziuze wenyewe na kunufaika na uamuzi wa Rais Magufuli wa kuuza korosho kwa bei ya Sh 3,300 kwa kilo.