Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalam “Vibrio cholera”.
Chanzo cha ugonjwa huu.
Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.
Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi cha mtu bila yeye binafsi kuonyesha dalili zozote za ugonjwa.
Dalili za ugonjwa huu
Mgonjwa wa Kipindupindu huwa na dalili zifuatazo:
-Kuharisha mfululizo au mara kwa mara bila tumbo kuuma ambako kunaweza kuambatana na kutapika.
-Kinyesi au matapishi huwa ya maji maji yasiyo na harufu, yanayofanana na maji yaliyooshewa mchele.
-Kusikia kiu sana, macho kudidimia na ngozi kusinyaa ambavyo hutokana na upungufu wa maji mwilini.
-Kuishiwa nguvu, kuhema haraka haraka na kulegea. Hali hii hutokana na upungufu wa maji na madini mwilini.
Jinsi Kipindupindu kinavyoenea
Kula chakula au kunywa kinywaji chochote kilicho na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu kwa mfano:-
-Kunywa maji yasiyochemshwa.
-Kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira ambayo siyo safi.
-Kula matunda yasiyooshwa kwa maji safi na salama.
-Kunywa pombe za kienyeji zilizoandaliwa katika mazingira machafu au kunywea katika vyombo vichafu.
-Kula mboga za majani, kachumbari na saladi bila kupikwa au kuziosha kwa maji safi na salama.
-Kula chakula au kumlisha mtoto bila kunawa mikono kwa sabuni na maji safi na salama yanayo tiririka.
-Kuosha au kuhudumia mwili wa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa kipindupindu bila kujikinga.
-Kunawa mikono kwenye chombo kimoja kwa mfano ndani ya bakuli au beseni kabla ya kula chakula.
-Kutotumia choo au utupaji ovyo wa kinyesi.
-Kutonawa mikono baada ya kutoka chooni.
-Kuweka mazingira katika hali ya uchafu mfano kutupa taka ovyo bila kuzingatia kanuni za afya..
-Kula vyakula vilivyopoa na visivyofunikwa.
-Kutiririsha maji ya chooni ardhini na hivyo kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na chakula.