Wakazi wa Nairobi walazimika kutembea kwenda kazini


Mamlaka za jiji la Nairobi zimeanza kutekeleza sheria inayopiga marufuku magari ya usafiri wa umma maarufu kama matatu kuingia katikati ya jiji kuanzia leo.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa mamlaka inalenga kupunguza msongamano wa magari.

Sheria hiyo mpya ilianza kutekelezwa mapema alfajiri ya leo ambapo maafisa wa trafiki wa kaunti ya Nairobi walikuwa wakizuia matatu kuingia sehemu ya katikati ya jiji.

Baadhi ya maafisa hao waliokuwa wamejihami kwa silaha za moto wamepelekwa katika vituo vipya vilivyowekwa nje ya jiji

Maafisa hao waliweka vizuizi vya barabarani katika eneo la Muthurwa, barabara ya Murang'a, Fig Tree A, barabra ya Desai, barabra ya Ngara, Hakati, Railways na kituo kikuu cha mabasi katikati ya jiji.

Amri yao kwa wahudumu wa matatu ilikuwa wazi: "Simama! Hakuna kuendesha gari kupita hapa."

Maafisa hao walikuwa wanayazuia matatu yanayojaribu kuingia jijini kurejea yalikotoka au kutafuta njia nyingine mbadala.

Katika mzunguko wa uwanja wa michezo wa City, polisi waliegesha gari lao katika sehemu moja ya barabara ili kuyafungia magari yote ya usafiri wa umma yanayotumia barabara ya Jogoo.

Hali ilikuwa hiyo hiyo katika barabara kuu za Thika na Limuru , ambako wasafiri wengi walilazimika kushukia stendi ya Fig Tree katika eneo la Ngara .

Katika eneo la katikati ya jiji ambako barabara nyingi hushuhudia msongamano mkubwa saa za asubuhi hali ilikuwa tofauti.

Hapakuwa na matatu katika maeneo ya Koja, Odeon, Kencom, GPO, OTC, Commercial, Ronald Ngala , Ambassadeur, barabara ya Murang'a pamoja na vituo vingine vya mabasi ya River Road.

Alhamisi iiyopita wahudumu wa matatu walikuwa wameapa kukaidi amri hiyo hali iliyozua hufu ya wahudumu hao kukabiliana na maafisa wa kuweka usalama

Wamilikiwa matatu wanahoji kuwa Gavana wa jimbo la Nairobi Mike Mbuvi Sonko amekimbilia kuweka sheria hii mpya bila kuwashirikisha wadao wote husika katika suala hilo.