Wanaswa na vipodozi, pombe kutoka nje ya nchi

JESHI la Polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamewakamata wanawake wanne wakisafirisha bidhaa mbalimbali zilizopigwa marufuku kuingizwa nchini, vikiwamo vipodozi na pombe haramu.

Akizungumza na wandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ulrich Matei, alisema wanawake hao walikamatwa kwa nyakati tofauti ndani ya siku mbili.

Alisema katika tukio la kwanza, Betty Emmanuel (36) mkazi wa Nzovwe na Felister Jojo (38) mkazi wa Majengo B jijini Mbeya, walikamatwa katika eneo la Ituta Kata ya Iyunga jijini Mbeya.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Novemba Jumatano wiki hii 6:52 usiku wakisafirisha vinywaji aina ya Kungfu katoni 700 kutoka Zambia kuingia jijini Mbeya kwa kutumia lori aina ya Scania lenye namba za usajili T242 BPE.

Kamanda Matei alisema maofisa wa Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TRA Mkoa, walifanya uchunguzi na kubaini kuwa wafanyabiashara hao hawana leseni za kufanyia biashara na wala hawana risiti kwa ajili ya kuwapa wateja wao wanaponunua bidhaa zao.

“Kutokana na makosa hayo, watuhumiwa wametozwa faini na TRA ya Sh. milioni 6.879 kwa makosa ya kufanya biashara bila leseni pia kutotoa risiti kwa wateja pindi wanapowauzia bidhaa hizo,” alisema Kamanda Matei.

Katika tukio la pili, Kamanda Matei alisema Rabia Kagoma (42) na Tubuni Kagoma (45) wote wakazi wa Iyela jijini Mbeya, walikamatwa wakiwa na vipodozi vilivyopigwa marufuku pamoja na pombe kali.

Watuhumiwa hao, walikuwa na pombe kali aina ya Prince kutoka Malawi katoni moja, vipodozi aina ya Extra Claire katoni moja, OranVate Gel katoni mbili, Beauty katoni moja na Betasol Lotion katoni moja.

Alisema watuhumiwa walikuwa wanasafirisha pombe na vipodozi hivyo kwa kutumia gari lenye gari aina ya Scania lenye namba za usajili T.111 DCS na kwamba  wanaendelea kushikiliwa huku upelelezi ukiendelea.

Matei alisema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria huku akiwataka wananchi kuacha kujihusisha na biashara haramu.

Akizungumzia sakata hilo, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Davis Mwangate, alisema walifanya uchunguzi na kubaini kuwa vinywaji hivyo viliingia mpakani kwa kufuata taratibu lakini ushuru waliolipa walikadiriwa kidogo.

Alisema Kitendo walichokifanya wafanyabiashara hao ni sawa na uhujumu uchumi kwa sababu wameikosesha serikali mapato lakini pia wameingiza bidhaa ambazo zinaharibu soko la bidhaa za ndani.

“Kama mtu ana uwezo wa kuagiza katoni 400 huyo si mfanyabiashara mdogo tena hivyo wamelipia ushuru Sh. 300,000 lakini tukaamua kuwaongezea, hivyo kila mmoja tumemtoza Sh. milioni 3.5,” alisema Mwangate.

Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) Mkoa wa Mbeya, Grace Kapambe, alisema baadhi ya vipodozi vilivyoingizwa na wafanyabiashara hao vimepigwa marufuku kuingia nchini kwa sababu vina viambata sumu.

Alisema vipodozi hivyo vina madhara mbalimbali kwa watumiaji yakiwamo ya muda mfupi na muda mrefu hususan magonjwa ya ngozi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items