1/11/2019

Bondia mwanamke amdunda na kumdhibiti mwizi mwanaume

Mwanaume mmoja amejikuta katika wakati mgumu baada ya kujaribu kumuibia mwanamke mmoja nchini Brazil.

Hata hivyo, mwanamke huyo hakuwa wa kawaida bali bondia wa kimataifa wa mchezo wa mapigo mchanganyiko.

Bi Polyana Viana mwenye miaka 26 alikuwa ameketi nje ya nyumba moja jijini Rio de Janeiro siku ya Jumamosi kabla ya kijana mmoja kumkabili na kujaribu kukwapua simu yake.

Alipoona hali imebadilika na hatari inamnyemelea, bondia huyo alitumia ujuzi wake wa ulingoni kujinasua.

Mwanamke huyo alimvurumishia mvua ya makonde na mateke mwizi huyo na kumuangusha na kumdhibiti vilivyo kabla ya askari kuja kumuokoa.

"Aliniambia: 'Nipe simu yako. Usifanye kitu chochote sababu nina silaha'," Viana aliliambia jarida la MMA Junkie.

"Kisha akauweka mkono wake kwenye bunduki, lakini nikagundua kuwa ni laini sana.

"Nilipoona hivyo nikasimama. Nikamtandika ngumi mbili na teke. Akadondoka chini. Nikampiga kabali ya nguvu. Kisha nikamkalia kwa juu na kumdhibiti, nikamwambia, 'Sasa inabidi tusubiri polisi waje'."

Viana, ana rekodi ya kushinda mapambano 10 na kupigwa mara mbili. Pambano lake la mwisho lilikuwa Agosti mwaka jana ambapo alipigwa na JJ Aldrich.