Faida zitokanazo na kujisomea vitabu pekee


Ni watu wachache sana ndiyo wanaopenda na wanafahamu umuhimu wa kusoma vitabu. Watu wengi hasa Waafrika hawapendi kusoma vitabu ikiwa hakuna kinachowalazimisha kufanya hivyo kama vile mtihani, kazi, n.k.

Kwa hakika kuna maarifa mengi yaliyofichwa kwenye vitabu; hii ndiyo sababu watu wengi waliofanikiwa husoma au hata kuandika vitabu.

Ikiwa unataka kupata maarifa na kuboresha maisha yako kwa njia ya kusoma vitabu, basi fahamu faida  za kusoma vitabu.

1. Hukuongezea marifa mapya
Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi. Hivyo kwa kusoma vitabu unapata maarifa mbalimbali yaliyowekwa kwenye kitabu husika.

Hivi leo kuna vitabu vinavyohusu takriban kila kitu; kwa hiyo maarifa yoyote unayoyahitaji unaweza kuyapata kwenye vitabu.

2. Hukuwezesha kufikiri kwa kina
Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi; mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.

3.Hukuongezea uwezo wa lugha
Mbinu moja wapo ya kuongeza uwezo wa lugha ni kusoma machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha unayotaka kujifunza. Kwa kusoma vitabu utaongeza msamiati, utajifunza sarufi ya lugha au hata mbinu mbalimbali za matumizi ya lugha. Unachotakiwa kuzingatia hapa ni kusoma vitabu bora mara nyingi kadri uwezavyo.

4. Hukuwezesha kutumia muda vizuri
Unapotumia muda wako kusoma vitabu, ni wazi kuwa hutopata muda wa kupoteza. Kusoma vitabu kutakufanya utumie muda wako kuongeza maarifa yako zaidi.

5. Hukuwezesha kujenga hoja
“Fikiri kabla ya kuzungumza. Soma kabla ya kufikiri.”

Ni ukweli usiopingika kuwa Fran Lebowitz alifahamu wazi kuwa huwezi kuzungumza kabla ya kufikiri na huwezi kufikiri kabla ya kusoma. Kusoma kunakupa uwezo wa kufikiri na kujenga hoja zenye nguvu.

Ikiwa unataka kuzungumza ili watu wakuamini na wakusikilize, basi soma vitabu kila mara.

6.Hukuongezea ubunifu
Tofauti kubwa iliyopo kati ya kusoma vitabu na kuangalia televisheni ni juu ya kuongeza ubunifu wako.

Kadri unavyosoma vitabu, ndivyo unavyojifunza mambo mapya zaidi ambayo yatakufanya kuwa mbunifu. Kwa kusoma vitabu pia unaweza kufahamu jinsi watu wengine walivyotumia ubunifu kutimiza malengo yao pamoja na kukabili changamoto mbalimbali.


7. Hukuongezea uwezo wa kumbukumbu
Kadri unavyosoma vitabu ndivyo unavyoongeza uwezo wako wa kumbukumbu. Kwani kila mara unaongeza mambo mapya ambayo unatakiwa kuyakumbuka. Jinsi ubongo unavyopokea mambo mapya ndivyo unavyozidi kuongeza uwezo wake zaidi

Naamini sasa unakubaliana na mimi kuwa kuna vitu vya thamani sana vilivyofichwa kwenye vitabu ambayo watu wengi hawavifahamu.