Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imesaini mkataba wa mauzo ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa Kampuni ya Kenya ya INDO Power Solutions kwa malipo ya Shilingi bilioni 418.
Mkataba huo umesainiwa jijini Arusha jana januari 30 kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Dkt. Hussein Mansoor kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Brian Mutembei, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya.
Tukio hilo la kihistoria lilishuhudiwa na Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Awali wakizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo Mawaziri hao wakiongozwa na Prof. Kabudi, kwa pamoja walipongeza kwa dhati uamuzi wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Serikali kununua korosho kutoka kwa wakulima ili
kuepusha wakulima hao kuuza korosho zao kwa bei ya chini kwa watu wasio kuwa nania njema kwa wakulima.