Mwaka 2012 Uruguay ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuruhusu matumizi ya bangi kwa lengo la kujiburudisha, pia kuiwezeaha serikali kushughulikia biashara haramu na magenge ya wahalifu waliokuwa wanaiongoza biashara hiyo.
Haikuchukua muda wapiga kura katika majimbo mawili ya Washington na Colorado nchini Marekani kuunga mkono uidhinishwaji wa matumizi ya bangi ambayo si ya kimatibabu. Majimbo manane mengine kwa pamoja na Washington DC, yameunga mkono uhalalishwaji wa bangi kwa njia ya kujiburudisha.
Hadi matumizi ya bangi kwa minajili ya dawa yamekubaliwa katika majimbo 33 kati ya majimbo 50 nchini Marekani. Nchini Mexico serikali imewasilisha muswada bungeni ambao utahalalisha matumizi yake kama dawa na burudani licha ya mahakama kuu kupiga marufuku kwa kile ilichoeleza ni kinyume cha sheria.
Nchini Uhispania ni ruhusa kuvuta bangi japo kwa siri, ilihali dawa hizo zinauzwa wazi katika maduka yenye majina Coffee Shops nchini Uholanzi.
Kwa upande wa Uingereza, madaktari wamekubaliwa kuwapa wagonjwa bidhaa za cannabis tangu mwezi Novemba.Korea Kusini wamehalalisha matumizi ya bangi kama dawa lakini chini ya mazingira yenye sheria kali, licha ya kuwahukumu wakaazi wanaotumia dawa hizo hata nje ya nchi.
Tukija barani Afrika, Lesotho ilikuwa nchi ya kwanza kuruhusu kilimo na matumizi ya bangi kwa sababu za kiafya tu. Pia Aprili mwaka jan, Zimbabwe ilikuwa nchi ya pili kuhalalisha uzalishaji wa bagi kwa matumizi ya kiafya na kisayansi.
Utakumbuka Septemba mwaka jana Mahakama ya Kikatiba nchini Afrika Kusini ilihalalisha utumiaji wa bangi kwa watu wazima katika maeneo faragha.
Hadi kufikia hapo ni dhahiri kuwa mataifa mengi yatafuata mkondo huo, maswali yanayoibuka ni kipi nyuma ya pazia kuongezeka kwa nchi zinazohidhinisha matumizi ya bangi. Je, ni nini hasa kinachopelekea mataifa mbalimbali kulegeza kamba kwenye sheria zake, au hata kuidhinisha matumizi ya bangi?

