Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema tatizo la Utakatishaji Fedha haramu linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana nalo kwani linahatarisha Maendeleo ya Mataifa mengi duniani.
Jaji huyo amesema tatizo hilo linapelekea taifa kupoteza heshma yake na kutoaminika mbele ya mashirika na jamii ya kimataifa na kuzorotesha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Jaji Makungu alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Majaji, Mahakimu na Makadhi wa Zanzibar namna ya kushughulikia masuala ya fedha haramu yanayofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi.
Amesema utakatishaji fedha haramu ni vitendo vya aibu na vinahatarisha mfumo mzima wa fedha katika nchi, sheria na usalama hatimae nchi kupoteza washirika wake wa maendeleo.
Alisema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali ikiwemo kutunga sheria ya kukabiliana na vitendo hivyo viovu.
Aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa jitihada za pamoja zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na tatizo hilo zimeleta mafanikio makubwa.
Alisema vitendo vya uhalifu na dawa za kulevya, ambavyo ni miongoni mwa mambo yanayopelekea utakatishaji wa fedha haramu vimekua vikidhibitiwa na kupungua kwa kiasi kikubwa.
