Serikali imesema kuwa itawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika katika mauaji ya watoto mkoani Njombe.
Akizungumza Bungeni leo, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Kangi Lugola amesema tayari wameshabaini baadhi ya wale waliohusika na mauaji hayo na hatua kali zitachukuliwa.
"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina. Tayari tumeshawabaini baadhi ya wale ambao wameshiriki. Nawataka watu waache kuichezea serikali," amesema Lugola.
Hivi karibuni Watoto sita, wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 wamepatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha mkoani humo.
