Tafiti za Kisayansi zinasaidia vyanzo vya maradhi - Dkt. Hussein Mwinyi


Na.Thabit Madai,Zanzibar.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi amesema tafiti za Kisayansi za Afya zinasaidia kujua chanzo cha maradhi na tiba yake ikiwemo matumizi ya dawa asilia.

Dk.Husein alieleza hayo Binguni Wilaya ya Kati Unguja wakati wa Ufunguzi wa Jengo la Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI) ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema tafiti za kisayansi ya afya katika nchi zinamchango mkubwa katika kupunguza maradhi kwani baadhi ya maradhi yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia vyakula vya kawaida bila kutumia dawa za Hospitali.

Aliwataka wananchi kupokea matokeo ya tafiti zitakazofanywa na Taasisi hiyo na Taasisi nyengine ili kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Dkt. Hussein aliwashauri wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na  kuhakikisha mimea na dawa za asili zinazotumika kwa ziko katika hali ya usalama kwa matumizi ya binaadamu.

Alieleza kuwa shabaha ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kumkomboa mwananchi na madhila mbali mbali yakiwemo maradhi na kuwafanya wawe na afya bora. 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla lisema lengo la kuanzishwa Taasisi hiyo ni kufanya tafiti kujua ukubwa na chanzo cha maradhi maradhi na kushirikiana na Taasisi nyengine kutoka nje ili kupata tiba sahihi. . 

Alisema zaidi ya shiling million mia mbili zimetumika katika ujenzi wa jengo la Taasisi ya Utafiti ya afya Zanzibar lenye wafanyakazi 21 na mipango ya kuajiri wataalamu wa fani ya utafiti zinaendelea kuchukuliwa ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

 Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja Mashavu Sukwa aliitaka Wizara ya Afya kuangalia uwezekano wa kuwachukua wananchi wa karibu kufanyakazi ndogo ndogo zisizohitaji utaalamu katika Taasisi hiyo na kushirikishwa katika ujenzi wa hospitali ya rufaa itakayojengwa kijijini hapo.

“Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wapo tayari kufanyakazi mbalimbali wakati wa ujenzi wa Hospitali ya Binguni kwani wako imara katika kazi zinazohitaji nguvu," alisema Mkuu wa Wilaya ya Kati

Mfamasia Mkuu wa Serikali Habibu Ali Sharifu alisema suala la utafiti linawahusu wananchi wote wa Zanzibar hasa katika  kupunguza matumizi ya dawa bila mpangilio na hatimae kusababisha athari.

Aliwashauri wananchi wa Binguni kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar kwani wanamchango mkubwa kufanikisha kazi za Taasisi hiyo

Alisema wananchi wakipewa  elimu ya matumizi ya njia mbadala za tafiti za kisayansi zitasaidia kuondoa mawazo potofu na kupata matokeo chanya ya tafiti zilizofanya na wataalamu.