1/11/2019

TAMWA yapata Mkurugenzi Mpya


Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimemtangaza Rose Rueben kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake mpya kujaza nafasi inayoachwa wazi na Edda Sanga, anayemaliza nafasi yake.

Mkurugenzi huyo mpya amekabidhiwa ofisi rasmi leo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za Tamwa zilizopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama mbalimbali wa chama hicho.

Dk. Rose Ruben aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam, sasa TBC Taifa, Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), kabla ya kuamua kuachana na shirika hilo na kufanya shughuli zake binafsi huku akiendeleza harakati za kumkomboa mwanamke na watoto.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa wadhifa wa kuongoza taasisi hiyo,Rose alisema: "Nitaendeleza harakati za kumkomboa mwanamke na watoto, kupinga ukatili wa kijinsia, kufanya kazi kwa kufuata katiba, kanuni na sheria za nchi ili tusitoke nje ya sheria za nchi yetu," naomba tushirikiane kuhakikisha Tamwa inasonga mbele, tuchape kazi kwa maendeleo ya Tamwa na jamii ya watanzania wanaotuzunguka, hapa kazi tu.

Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo,Tamwa inatekeleza mradi wa kupinga ukatili kwa watoto na wanawake katika wilaya saba lakini chini ya uongozi wake atahakikisha mradi huo unatekelezwa Tanzania nzima.