Bunge la Marekani lataka msaada wa Marekani kusitishwa Yemen


Baraza la wawakilishi nchini Marekani limeidhinisha Februari 13 mwaka huu azimio litakalofikisha mwisho uungaji mkono wa Marekani kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita nchini Yemen.

Hatua hiyo imechukuliwa wakati wabunge wengi  wakitaka kumlazimisha rais Donald Trump  kuimarisha sera  zake  kuelekea  nchi hiyo  ya  Kifalme.

Ilikuwa  mara ya  kwanza  baraza hilo la wawakilishi kuunga  mkono azimio  la  madaraka  ya  vita, lakini  kura hiyo  iliyoungwa  mkono  na wabunge  248 kwa  177 waliopinga, kwa  karibu kwa  misingi ya kichama, haitatosha, hata hivyo, kuweza  kuikiuka  ahadi  ya  Trump kutoa kile  ambacho  kinaweza  kuwa  kura  yake  ya kwanza  ya  turufu.

Wabunge 18 tu wa chama  cha  Trump  cha Republican  katika  baraza  hilo  la  wawakilishi  waliojiunga na  Wademokrati 230 kuunga  mkono  azimio  linalotaka kuzuwia  jeshi  la  Marekani  kujiingiza  katika  uhasama ndani  ama  inayoiathiri  Yemen, ikiwa  ni  pamoja  na kutoa msaada  wa  kujaza  mafuta  katika  ndege  zinazofanya mashambulizi  katika  vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe nchini  Yemen, bila  ya  idhini  kutoka  katika  bunge  la Marekani  Congress.