CHADEMA wamvaa Dkt. Molleli shambulio la Lissu, wataka Polisi wamuhoji


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema ushahidi uliotolewa na Mbunge wa Siha, Dkt. Godwin Mollel bungeni kuhusu shambulio la Tundu Lissu haupaswi kupuuzwa.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema Jeshi la Polisi linapaswa kutumia kauli ya Dkt. Mollel kama sehemu ya kuanzia ili wafungue upya jadala la Uchunguzi.

February 8 mwaka huu Bungeni Jijini Dodoma, Aliyekuwa Mbunge wa CHADEMA, Dkt. Godwin Mollel (sasa Mbunge wa CCM, Siha) alisema Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi ni mpango uliosukwa na CHADEMA.

"Mimi nilikuwa huko lakini nilikimbia kwa mipango yao, hata katika tukio la kushambuliwa Lissu mimi niliingia ndani kwenye uchunguzi na niliiba baadhi ya vitu lakini wakakataa mapendekezo yangu," alisema Molllel.

Utakumbuka Septemba 17, 2017 Tundu Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa risasi
akitokea Bungeni Jijini Dodoma. Lissu alipatiwa matibabu ya mwanzo nchini Kenya kisha kuhamishiwa Ubelgiji ambapo hadi sasa anapatiwa matibabu licha ya kufanya ziara kwenye nchi mbalimbali.