Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Meru, Baba Elias Kitoi Nassari amepongeza kampeni ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa inayofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Ndugu Jerry Cornel Muro ambapo amesema kanisa mbali na kupongeza linaunga mkono jitihada hizo.
Askofu Nassari amezungumza hayo leo alipomtembelea Mkuu wa wilaya ya Arumeru ofisini kwake kwa lengo la kumpongeza kwa kazi Kubwa anayoifanya katika sekta ya Elimu na Afya uku akiwa ameambatana na Uongozi Mkuu wa kanisa Dayosisi ya Meru akiwepo Mchungaji Ndelekwa Kuvavanael Pallangyo Msaidizi wa Askofu, Ndugu Lazaro Andrew Katibu Mkuu wa Dayosisi na Ndugu Elisate Manyaeli Maturo Mtunza Hazina Wote ni kutoka KKKT Dayosisi ya Meru.
Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru Baba Askofu Nassari amemkabidhi Lori lililoleta shehena ya mifuko ya saruji Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika halmashauri ya Meru.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arumeru Ndugu Jerry Muro mbali na kupokea pongezi na salamu za Kanisa, ameshukuru msaada wa shehena ya mifuko ya saruji iliyotolewa na kanisa, ambapo amemuhakikisha Baba Askofu Nassari kuwa Serikali ya wilaya ya Arumeru itaendelea kushirikiana na kanisa katika sekta zote za utoaji wa huduma Kwa wananchi.
