Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amelaani vikali vitendo vya watumishi wa umma kutumia nguvu nyingi dhidi ya wananchi hali inayopelekea hata mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia.
Ameeleza hayo wakati wa mazishi ya marehemu Isaka Petro aliyefariki katika vurugu zilizotokea katika kanisa la Waadiventisti Wasabato Itigi kundi Namba Two na kuzikwa nyumbani kwao kijiji cha kazikazi kata ya Kitaraka.
“Hakuna namna tunaweza kusema vinginenevyo kuhusu tukio hili zaidi ya kuwa tukio baya na la kusikitisha sana kuwahi kutokea kwa wananchi wetu, tena likiwa limetekelezwa na watumishi wa Serikali inasikitisha sana nawasihi watumishi wa umma tutangulize utu mbele katika kila kazi tunazozifanya”
Waziri Jafo ameendelea kwa kusema kuwa watumishi wa umma haijalishi unafanya kazi gani katika mazingira na hali gani lakini wanatakiwa kutanguliza ubinadamu kwanza ili kulinda maisha yao na wa wale wanaowahudumia.
