Jumanne hii,ilikuwa ni siku ya maswali na majibu bungeni mjini Dodoma ambapo wabunge mbalimbali wameuliza maswali na kujibiwa na serikali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMUSHI WA UMMA NA UTAWALA BORA, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa;
1. Katika mwaka wa fedha 2017/18, kupitia wizara, idara zinazojitegemea na wakala, Serikali ilitenga Sh. 54,470,327,822 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya ndani na nje kwa watumishi wa Umma.
2. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya Sh. 39,839,347,632 zimetengwa kwa ajili hiyo.
3. Serikali imeimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo hususani Australia, India, Japan, China, Indonesia, Jamhuri ya Korea ambapo katika mwaka 2016/17 kupitia wadau hao jumla ya watumishi wa Umma 654 walipatiwa mafunzi ya muda mfupi na mrefu katika nchi hizo.
4. Katika mwaka 2017/18 fursa za mafunzo zilizotolewa na washirika hao ziliongezeka hadi kufikia 827.
5. Fursa hizo zimewezesha watumishi wa Umma kupata uelewa, ujuzi na maarifa mapya ya kumudu majukumu yao katika kutekeleza malengo ya Taifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA, Mhe. Antony Mavunde;
6. Serikali kupitia mradi wa MIVARF imevijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji Tanzania Bara na Visiwani ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji itakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.
7. Tarehe 3 Novemba, 2017, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) walisaini makubaliano ya uendeshaji wa Mfuko wa dhamana.
8. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali.
9. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilishatangaza utaratibu wa namna benki mbalimbali za biashara zinavyoweza kushiriki katika Mfuko wa udhamini ambapo benki za CRDB, NMB, TPB na PBZ zilionyesha nia.
10. Benki ya NMB na TPB wameshakubaliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kushiriki katika kutoa mikopo kwa vikundi vya wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana.


