Serikali imelitaka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) kusaidia katika utoaji wa vitambulisho kwa wakimbizi wote walioko katika makambi pamoja na kusaidia uanzishwaji wa kanzidata ya wakimbizi nchini itakayomilikiwa na serikali.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhnadisi Hamad Masauni wakati akizungumza katika kikao cha ndani na Ujumbe ulioongozwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) Fillippo Grandi,ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi.
Naibu Waziri Masauni alisema Serikali ya Tanzania imekua na historia ndefu katika jukumu la kuhifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi zao lakini wakimbizi hao wanatakiwa kutokua sehemu ya watu wanaovunja sheria pindi wawepo makambini.
“Ni muhimu sasa UNHCR wakasaidiana na serikali katika kuboresha orodha ya wakimbizi walioko nchini sambamba na ugawaji wa vitambulisho kwa wakimbizi watakaothibitika kisheria kuwa ni wakimbizi huku ikisaidia katika kupokea wakimbizi halali na sio wahamiaji haramu” Alisema Masauni
Akizungumza katika kikao hicho Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani(UNHCR) Fillippo Grandi aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kupokea wakimbizi kwa muda mrefu na akiweka wazi lengo lao la kushirikiana na nchi zinazopokea wakimbizi katika kusimamia zoezi la urejeshwaji wa wakimbizi wanaotaka kurudi kwao kwa hiyari
“Tutahakikisha tunasimamia wakimbizi kutii sheria za nchi husika ikiwemo uhifadhi wa mazingira katika makambi na kusaidia urejeshwaji wa wakimbizi walio tayari kurejea katika nchi zao baada ya kurejea kwa amani” alisema Filippo
Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi Laki Tatu katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli zilizopo mkoani Kigoma.
