Timu za Afya Mikoa yote nchini watakiwa kujitathmini


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, anayeshughulikia afya, Dkt. Dorothy Gwajima, ameziagiza timu za Afya za Mikoa (Regional Health Management Team- RHMT) yote nchini, kujitathmini hali yao ya utendaji kazi na kuona kama wanatija inayokubalika kwa taifa.

Gwajima ameitoa kauli hiyo, alipokuwa akizungumza na timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma inayo ongozwa na James Kiologwe, Mganga Mkuu wa Mkoa huo wakati alipofanya ziara yake ya kwanza toka ateuliwe kushika wadhifa huo Januari 8 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Akiwa katika ziara hiyo, Gwajima alisema kila mmoja katika timu hiyo inayo simamia afya wajifanyie tathmini dhidi ya utendaji wao huku akisema, ametumia jukwaa hilo la timu ya Dodoma  na waliopo katika Mikoa Mingine yote nchini nao wajitathmini huko huko walipo wasingojee ziara yake ndio waanze kubadilika.

“Tatizo kubwa tulilonalo ni uratibu wa kazi, jukumu moja unakuta linakuwa na uratibu usiofahamika jambo ambalo wakati mwingine hata mtekelezaji anashindwa afanye lipi na aache lipi'' alisema Gwajima

Pia amesema kuwa, hili ndilo alilogundua ndani ya siku zake 30 za kuwepo katika Ofisi yake mpya,
Timu za Afya za Mkoa zimetakiwa kutambua kwamba, majukumu yao ndio maduka yao wanaotakiwa kuyafanyia kazi usiku na mchana huku wakionesha matokeo chanya ya kile wanancho kifanya kwa kutoa taarifa kwenye ngazi husika.

Gwajima amesisitiza kwamba katika dira aliyonayo kwenye kutekeleza majukumu yake mapya ni pamoja na kuzingatia, uratibu (Cordination), matokeo chanya (Result/Productivity), huduma bora (Good Services) kwa mteja pamoja na kuwajali wateja (Customer care), hivyo akawataka wajumbe wa timu zote za afya za mikoa Tanzania Bara, kulijua hilo na kulizingatia.

“Inatia hofu sana, unakuta mtu ni mratibu wa kitengo fulani katika ngazi ya Mkoa, lakini hata siku moja hajafanya ziara wilayani kwenda kujionea changamoto zilizopo na kushauri nini chakufanya, mimi niwaambie wakati nikiwa Mganga Mkuu wa Wilaya kuna mambo tulikuwa tunaibua katika ngazi ya wilaya na badae yanakuwa na maamuzi kwenye ngazi ya taifa” alisema Gwajima.

Gwajima akawataka wajumbe wote wa timu za mikoa kufanya kazi kiteknolojia ili kuongeza tija ya utendaji kazi wao lakini pia matumizi ya teknolojia iwe ni chachu ya wao kufanya kazi na kuonesha matokeo (Productivity).

Dkt. Dorothy Gwajima aliteuliwa kushika wadhfa huo wa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya OR-TAMISEMI, akichukua nafasi iliyo achwa wazi na Dkt. Zainab Chaula aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya nah ii ni ziara yake ya kwanza kufanya katika Sekretarieti ya Mkoa.