Na Thabiti Madai, Zanzibar
Ujenzi wa kituo kikuu cha daladala Kijangwani unatarajiwa kuendelea mapema mwezi Febuari kwa kuwekwa lami na miundombinu mengine ambapo mara tu utakapokamilika kituo hicho kitaanza rasmi kutoa huduma kwa wasafiri.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud hapo Ofisini kwake Vuga, mbele ya waandishi wa habari waliotaka kujuwa juu ya mradi wa CCTV Camera na vituo vya daladala katika Mkoa huo na kusema kuwa tayari mkandarasi wa ujenzi wa kituo hicho ameshapatikana.
Amesema mbali na kituo hicho Mkoa una mpango wa kujenga vituo vidogo vidogo vya daladala katika barabara kuu ndani ya Mkoa huo na pale Serikali itakapopitisha mpango huo ujenzi wake utaanza.
Aidha amesema kuwa Serikali itajenga vituo vyengine vikubwa vya daladala na gari za shamba sambamba na masoko nje ya mji ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wakaazi wake pamoja na kupunguza msongamano katikati ya mjini.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amewahakikishia wananchi kuwa daladala zitaendelea kusafirisha abiria hadi Hospitali kuu ya Mnazimmoja na vituo vidogodogo vinavyotumika sasa wakati kituo kikuu cha daladala cha Kijangwani kitakapofunguliwa, hata hivyo gari hizo hazitaruhusiwa kuegeshwa kusubiri abiria katika vituo hivyo vidogo.
Akizungumzia kuhusu mradi wa CCTV camera Mheshimiwa Ayoub amesema tangu mradi huo uanze kufanya kazi umesaidia sana kubaini wezi wa vyombo vya moto, vitendo vya utekaji nyara na uhalifu ambapo zaidi ya watu saba walikamatwa. Vilevile ameeleza kuwa camera za CCTV zimewezesha kupata taarifa za kipelelezi kwa haraka pamoja na kupata ushahidi wa matukio ya kihalifu na uvunjifu wa sheria barabarani.
