Ukweli kuhusu dawa ya kutibu uzee


Teknolojia ya Seli Shina (Sterm Cell) ambayo inatumia chembechembe za seli za mwanadamu kutibu kiungo chochote katika mwili husika, inatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa mpaka yasiyoambukiza yakiwemo saratani zote, utindio wa ubongo, seli mundu, kisukari, ualbino na kupooza.

Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, alibainisha tiba hiyo ya seli shina ina uwezo mkubwa na tayari imethibitika duniani kumrudisha mtu aliyefika hatua ya uzee kuwa kijana mwenye afya njema.

Dk. Mengi kupitia kampuni yake ya IPP - Utafiti, Teknolojia na Ugunduzi, akishirikiana na wataalamu mbalimbali duniani, amesema ataanzisha maabara hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni upatikanaji wa vibali kutoka serikalini.

Alisema kuanzishwa kwa maabara hiyo hakuna maana kwamba anapingana na uumbaji wa Mungu kuwa ni lazima binadamu afe, lakini lengo ni kuhakikisha wale wanaopitia maumivu na tabu kubwa kutokana na kukosa tiba ya magonjwa yanayowasumbua yakiwemo yanayotokana na umri mkubwa wanapata tiba hapa hapa nchini.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema serikali haina tatizo juu ya hilo, kwa sababu ni maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya nchini na kumtoa hofu Dk. Mengi kuwa vibali hivyo vitapatikana haraka.