.

2/14/2019

Wahandisi watakiwa kukesha site ujenzi wa Hospitali ya Wilaya


Na James Timber, Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wahandisi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela kushirikiana pamoja na  kuweka kambi usiku na mchana eneo la inapojengwa hospitali ya wilaya hiyo mpaka ujenzi huo utakapokamilika.

Rai hiyo ameitoa akiwa mtaa wa Kabusungu kata ya Sangabuye kwenye eneo la ujenzi wa hospitali, Inayotarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu kutoka sasa na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni mia tano kwa awamu ya kwanza ikitumika kujenga majengo saba likiwemo jengo la kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje, jengo la utawala, jengo la huduma za mama na mtoto, jengo la kujifungulia, jengo la mionzi, jengo la maabara na jengo la kufuria ambapo amewaasa wahandisi hao kuzingatia ubora, ufanisi na maelekezo sahihi ya matumizi ya fedha za ujenzi huo

"Lengo letu ni kurahisisha huduma muhimu kwa wananchi, waipate kwa ukaribu na kwa gharama nafuu hasa maeneo ya kando ya mji ambayo yamekuwa yakisahaulika sana, Lazima tukeshi site mpaka hospitali hii itakapokamilika," alisema.


Aidha Dkt Mabula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha sekta ya afya kwa ujenzi wa vituo vipya vya afya zaidi ya 300 mpaka sasa, hospitali za wilaya zaidi ya 60, kuongeza bajeti ya wizara hiyo mpaka kufikia zaidi ya bilioni 898, huku akiasa kutumia nguvu kazi ya wananchi wanaoishi jirani na mradi huo katika kutekeleza majukumu ya kila siku mpaka kukamilika kwa mradi.

Kwa upande wake muhandisi wa manispaa ya Ilemela Musa Maroba mbali na kuahidi kutumia nguvu kazi ya wananchi jirani amemuhakikishia mbunge huyo kukamilika kwa wakati kwa mradi huo kwani fedha zote zipo na wako teyari kufanya kazi usiku na mchana, kufa na kupona ili kwenda sambamba na muda uliotolewa sanjari na kuzingatia viwango vinavyotakiwa huku akitaja changamoto ya maji inayoendelewa kufanyiwa kazi na muhandisi wa maji wa wilaya hiyo ili kutokwamisha mradi huo.