Wamiliki wa Viwanda vya Misitu Tanzania wamehakikishiwa kuwa watashughulikiwa ombi lao la kutaka kuongezewa muda wa Mikataba yao kutoka miaka miwili hadi mitano ya kupewa mgao wa vitalu vya miti.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe. Constantine Kanyasu na
ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa Ofisini kwake na wamiliki hao yakiwemo ya gharama za tozo ya ushuru wa mazao ya misitu (Cess) inayotozwa na Halmashauri za Wilaya ya Mufindi ambayo licha ya Serikali kutoa maagizo ya kuzuia tozo hiyo bado wadau hao wanaendelea kutozwa.
Mhe. Kanyasu ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania (SHIVIMITA) na Wanachama wa Shirikisho hilo waliomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa SHIVIMITA, Ben Sulus amemuomba Naibu Waziri aangalie namna ya kuwasaidia wadau hao waongezewe muda wa Mikataba kutoka miaka miwili hadi mitano ya kupewa mgao wa vitalu vya misitu ili waweze kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za Kifedha kwa ajili ya kuendeshea viwanda vyao.
