Wananchi watulizwa kisa ardhi


TIMU ya Mawaziri wanane wanaotembelea maeneo ya migogoro ya ardhi nchini imewataka wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kutatua migogoro hiyo inayowakabili katika maeneo yao.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwandoya Wilayani Meatu mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa timu hiyo, William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema Rais John Magufuli ameunda timu hiyo ili kupitia migogoro ya hifadhi na kero za ardhi zinazowakabili wananchi nchi nzima.

Aliwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati timu hiyo ikikusanya malalamiko ya wananchi na kuyafikisha kwa Rais na baadaye yatatolewa uamuzi.

Alisema kufuatia agizo la serikali la kurejesha vijiji 366 vilivyokuwa vimependekezwa kufutwa, Rais Magufuli amesimamisha zoezi la kuwahamisha wananchi katika maeneo yao, huku akiwataka waliowekewa alama ya kuhama waendelee kuishi bila hofu.

"Rais amesimamisha zoezi la kuhamisha wananchi kwenye vijiji 366 ambavyo vilisajiliwa na serikali hiyo hiyo inayotaka viondoke, tutapitia maeneo yaliyotajwa ili kubaini mpaka wa pori na vijiji,” alisema na kuongeza:

“Maliasili walichukua maeneo bila kushirikisha wananchi, zoezi lolote litakaloendeshwa na Maliasili lazima liwe shirikishi kwa sasa.”

Alisema awali maombi ya wananchi yalikuwa ni kupewa kilomita 10 kutoka kwenye mpaka wa hifadhi na pori la akiba la Maswa kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.