3/18/2019

Baada ya Maalim Seif kuhamia ACT-Wazalendo, Mbunge Bwege afunguka


Na. Ahmad Mmow, Nachingwea

Mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini,Selaman Bungara(Bwege),amesema hajaamua achukue na kufanya uamuzi gani baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa CUF,Seif Sharrif Hamad kuhamia chama cha ACT- Wazalendo.

Akizungumza na Muungwana Blog kutoka Dodoma, Bwege ambaye inatajwa alikuwa upande wa Maalim Seif wakati wa mgogoro wa uongozi ndani wa chama cha CUF amesema hajamua afanye nini baada ya Muasisi huyo wa CUF kutimkia ACT-Wazalendo.

Alisema alichofanya Maalim Seif ni uamuzi wake, sio vikao halali vya chama. Kwahiyo hata kitendo chake cha kuwaomba wanachama wengine wa CUF wamfuate ACT ni mawazo yake binafsi.

"Yeye amewaomba wanaotaka mabadiliko ya kweli wamfuate alikohamia ili wakashirikiane kutafuta mabadiliko hayo.Ameomba sio amri, Kwahiyo ni uamuzi wa mtu binafsi kukubali au kukataa ombi lake,"alisema Bwege.

Mbunge huyo aliongeza kusema kwamba kufanya uamuzi katika jambo zito na kubwa kama la kuhama chama kunahitaji tafakari ya kina na umakini mkubwa. Uamuzi ambao hauhitaji kukurupuka na kufanya.

"Nimapema sana kusema nitafanya nini. Lakini kwakuwa imetokea hivyo nilazima nitafanya uamuzi  kwa wakati na sababu sahihi.Nasio mimi tu,bali wengi wanatafakari ili wafanye uamuzi sahihi baada ya kutokea hali hii,"aliongeza kusema Bwege.

Leo aliyekuwa katibu mkuu na muasisi wa CUF-Chama Cha Wananchi,Maalim Seif Sharrif Hamad
 kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii amekipa mkono wa kwaheri chama hicho na kupiga hodi ACT-Wazelendo.