Familia kupewa udongo kwa ajili ya maziko waliokufa ajali ya Boeing 737 MAX 8


Wafanyikazi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa nchini Ethiopia wamekusanyika Jumapili hii kuwakumbuka wahudumu waliokuwa katika ndege ya abiria Boeing 737 MAX 8  iliyoanguka Jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu  wote 157.

Wakiwa wenye huzuni na wakiangua vilio, wafanyikazi hao wameonekana wakiwa na mashada ya maua lakini pia mishumaa kama ishara ya kuwakumbuka wenzao.

Makanisani, ibada za kuwakumbuka raia wa nchi hiyo waliopoteza maisha pia imefanyika huku viongozi wa dhehebu la Coptic, wakionekana kuwatia moyo jamaa, ndugu na marafiki walioshindwa kujizuia, wakikumbuka kuondokewa na wapendwa wao.

Nayo serikali ya Ethiopia imesema familia zilizopoteza wapendwa wao, zitakabidhiwa mfuko wa udongo kutoka katika eneo lililotokea ajali hiyo kwa ajili ya mazishi kwa sababu hakuna mwili uliopatikana. Hata hivyo imesema familia zitapokea mabaki ya wapendwa wao baada ya uchunguzi ambao unatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita.