Faru 12 kuingizwa Nchini


Jumla ya Faru 10 wanatarajiwa kuingizwa nchini na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Grumeti Fund lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wanyama hao hapa nchini.

Kuagizwa kwa Faru hao kutaongeza idadi yao kutoka 2 walioagizwa na taasisi hiyo hapo awali hadi kufikia 12.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda kwenye kikao kilichowahusisha wadau hao wa uhifadhi kilichofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Pasiansi jijini Mwanza,

Amesema ongezeko la faru hao kutaboresha kizazi cha wanyama hao ambao wapo hatarini kutoweka
Amefafanua kuwa idadi hiyo itafanya faru hao kuongezeka kwa kuzaliana na wale waliopo nchini. Prof. Mkenda amewa hakikishia wadau hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika shughuli za kuimarisha uhifadhi nchini.

Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda ameishukuru Taasisi ya Grumeti Fund kwa kusaidia kuwaleta watu maarufu kutoka mataifa mbalimbali Duniani kuja nchini kutembelea hifadhi za Taifa na hivyo kuchangia kutangaza utalii na kuongeza pato la Taifa. Akizungumzia kuhusu ujio wa Faru hao, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Canisius Karamaga amesema kuwa jitihada zinazofanywa na Taasisi hiyo zinalenga kuongeza idadi ya Faru hapa nchini.

Amesema Faru hao mara baada ya kuingizwa nchini watatunzwa na kulindwa kwa ushirikiano ili wasiweze kuuawa na majangili.

Aidha, Amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda Maliasili zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.