Ifike mahala tufikirie kusimamia miradi kwa uadilifu - Waziri Kamwelwe


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amewataka watendaji wa Sekta ya Uchukuzi kufanya kazi kwa uzalendo na weledi katika usimamizi wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuleta maendeleo nchini.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Sekta hiyo na kusema kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi katika miradi mikubwa ikiwemo ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), ukarabati na ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge) hivyo, haitamvumilia Mtendaji yoyote atakayehujumu miradi hiyo.

“Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye Sekta hii, hivyo ifike mahala tufikirie kusimamia miradi hii kwa uadilifu na uzalendo kwani uongozi unahitaji malengo ili kufanikisha utekelezaji’, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe, amewapongeza Wakuu wa Taasisi zinazosimamiwa na sekta hiyo kwa kusimamia miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini.

Aidha, Waziri Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimeibuliwa na wadau wa usafirishaji katika utekelezaji wa Sheria mpya ya Uzito wa magari na kusema kuwa Serikali haitarudi nyuma juu ya sheria hiyo kwani inafanya hivyo ili kuilinda miundombinu ya barabara nchini.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items