3/17/2019

Kocha wa Simba SC aeleza hawakuwa na chaguo zaidi ya kupata ushindi


Baada ya Simba SC kupata ushindi mbele ya wapinzani wao AS Vita kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Uwanja wa Taifa Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems amesema kuwa hawakuwa na chaguo jana zaidi ya kupata ushindi.

Simba imetinga hatua ya robo fainali Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 jambo ambalo limewafurahisha mashabiki wa Simba na Taifa kiujumla.

Aussems amesema ilikuwa ngumu kwake kupoteza na hakufikiria kushindwa kutokana na nguvu ya kundi hasa kwa namna linavyopata matokeo kwenye michezo ya kimataifa.

"Ukiangalia namna ilivyokuwa kwa timu nyingi hasa kwenye kundi letu hatua ya makundi zilikuwa zinapata pointi nyumbani, sasa kama wao waliweza kwa nini iwe ngumu kwetu kushinda? Hivyo niliwaambia wachezaji hawana kazi mpya Uwanjani zaidi ya kushinda na ndicho kilichotokea.

Kocha huyo ameongeza kuwa Mabao mengi walifungwa ila wao hawakuwa na presha hesabu ilikuwa ni pointi tatu, mashabiki wa Simba na Taifa kiujumla wamefanya jambo jema na wanajivunia kupenya hatua hiyo muhimu.