Maofisa wa TRA watupiwa lawama na Wananchi, Kisa?


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imetadharisha wananchi wakiwemo wafanyabiashara kuwa kuna matapeli wanaojifanya maofisa wa mamlaka hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, tangu Disemba mwaka jana kumekuwa na malalamiko ya watu kutapeliwa.

Amesema, matapeli wamekuwa wakipigia watu simu na kujifanya maofisa wa TRA na wengine wanakwenda kwa wafanyabiashara na kuwatisha kwa lengo la kujipatia fedha.

"TRA ina utaratibu wake wa kuwasiliana na wafanyabiashara kwa utaratibu rasmi na kuwajulisha siku rasmi ambazo maofisa wetu watakwenda kufanya ukaguzi na unafanyika kwa uwazi bila vitisho na si kwa taratibu nyinginezo,"amesema Kayombo.

Amesema, wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa maofisa wa TRA wanawatapeli na kwamba, hali hiyo inaonekana kuota mizizi na linaharibu jina la mamlaka hiyo.

"Kama mtu atapigiwa simu au kama una mtu una wasiwasi nae tafadhali toa taarifa kwa ofisi zetu zilizopo karibu nawe au toa taarifa kituoa cha huduma kwa wateja namba 0800780078 au 08800750075 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa moja usiku na utupe namba ya muhusika ili tuweze kufatilia,"amesema Kayombo.

"Pia kuna namba ya Whatsup ambayo unaweza kutoa taarifa au kuuliza chochote kupitia namba 0744233333 hii ni saa 24 maalum kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na kuwawezesha kulipa kodi kwa wakati,"amesema.

Katika hatua nyingine Kayombo amewataka wananchi kulipa kodi ya majengo kwa wakati badala ya kusubiri tarehe rasmi ya malipo hayo kuepuka usumbufu.